NEWS

Saturday 19 August 2023

DC Mashinji aipongeza Benki ya Azania kwenye Bonanza la Michezo na Maonesho ya Wajasiriamali Serengeti


Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vincent Mashinji (mwenye skafu katikati) akisikiliza maelezo ya mhusika kwenye banda la watengenezaji wa mvinyo kutokana na asali, wakati wa Bonanza la Michezo na Maonesho ya Wajasiriamali lililofanyika katika kata ya Morotonga wilayani humo jana.
--------------------------------------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Serengeti
----------------------------------------

MKUU wa Wilaya (DC) ya Serengeti, Dkt Vincent Mashinji ameishukuru na kuipongeza Benki ya Azania kwa kuwajali wananchi wa wilaya hiyo, hususan wafanyabiashara wadogo wadogo - kwa kuwapa mikopo yenye masharti na riba nafuu. 

DC Mashinji alitoa pongezi hizo wakati wa kilele cha Bonanza la Michezo, Burudani na Maonesho ya Wajasiriamali lililofanyika katika kata ya Morotonga, wilaya ya Serengeti mkoani Mara, jana. 

Alisema wananchi wana kila sababu ya kujivunia na kuchangamkia huduma zinazotolewa na Benki ya Azania kwa kuwa inamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100. 
Meneja wa Bima ya Afya Benki ya Azania Tanzania, Emmanuel Magoiga akizungumza wakati wa bonanza hilo. 

“Mashirika yetu ya Hifadhi ya Jamii na Bima ya Afya Tanzania ndiyo yanayoimiliki hii benki. Kwa hiyo tunapokwenda kufanya kazi na benki hii tunaenda kufanya kazi na benki yetu wenyewe, na ndio maana inatujali. 

“Tunazo pia benki za NMB na CRDB ambazo Serikali ni wanahisa, lakini ambayo ni ya kwetu ni Benki ya Azania, chako ni chako jamani, ina mpaka akaunti za kufungua bure,”alisema DC Mashinji ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha bonanza hilo. 

Naye Mwenyekiti wa Bonanza hilo, Musa Magasi Msety ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Morotonga, aliishukuru Benki ya Azania na wajasiriamali wote waliojitokeza kushiriki maonesho hayo. 

“Leo tumeshuhudia hamasa kubwa, hongereni mliofanikisha shughuli hii - wajasiriamali mliokuja bila kujali umbali, wanamichezo pamoja na wananchi wote, bila kusahau timu ya Wamaasai - hongera sana mmecheza kandanda ya kibabe na ya kuvutia. Michezo ni sehemu ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, hivyo tutaendelea kuitekeleza kwa vitendo," alisema Magasi. 
Wachezaji wa timu Wamaasai FC wakijadiliana jambo baada ya kuchapwa bao na Wakongwe FC katika bonanza hilo.

Kwa upande wake Meneja wa Bima ya Afya Benki ya Azania Tanzania, Emmanuel Magoiga ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya Azania Tanzania, Dkt Rhimo Nyansaho, alisema benki hiyo ni mshirika mkubwa wa shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali kwa vitendo. 

Hivyo alitumia nafasi hiyo kuhamasisha wananchi wa Serengeti kuitumia kwa huduma mbalimbali za kifedha, akisisitiza kuwa ndiyo inayotoa mikopo yenye riba nafuu zaidi nchini. 

Bonanza hilo ambalo lilihusisha michezo ya soka kwa wanaume na wanawake, riadha, ngoma za asili pamoja na shughuli za maonesho ya kiutamaduni, liliandaliwa na Jamii Amani Forum chini ya ufadhili wa Benki ya Azania. 
Mwenyekiti wa Bonanza hilo, Musa Magasi Msety akizungumza

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages