Kamishna wa Polisi Jamii Tanzania, CP Faustine Shilogile (wa tatu kutoka kulia mbele) katika picha ya pamoja na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Juma Chikoka (wa nne kutoka kulia), Maafisa wa Polisi na viongozi mbalimbali wa Serikali mjini Tarime, leo.
-----------------------------------------------
Na Mwandishi wa
Mara Online News
-------------------------
KAMISHNA wa Polisi Jamii Tanzania, CP Faustine Shilogile leo Agosti 3, 2023 amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Polisi Tarime Rorya, ambapo amefanya kikao na maafisa wa jeshi hilo, Mkuu wa Wilaya na wadau mbalimbali wa polisi jamii.
Katika kikao chake na Maafisa wa Polisi, Kamishna Shilogile amepokewa na Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Polisi Tarime Rorya, ACP Asifiwe Ulime - ambaye amemweleza kuwa hali ya usalama ndani ya mkoa huo ni shwari.
Kisha Kamishna Shilogile ametembelea ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, akapokewa na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Rorya, Juma Chikoka anayekaimu ofisi hiyo - ambaye alimweleza kuwa ushirikiano wa Polisi na jamii katika wilaya ya Tarime unaimarika kila siku kutokana na juhudi zinazoendelea kufanywa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, ACP Mark Njera pamoja na watendaji wake.
Aidha, DC Chikoka amempongeza Kamishna huyo wa Polisi Tanzania kwa ziara hiyo, akisema juhudi hizo za Jeshi la Polisi kuwafikia wananchi kwa ukaribu na kutoa elimu zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhalifu katika jamii.
Kamishna Shilogile ametumia nafasi hiyo kumkabidhi DC Chikoka vitabu vya mwongozo wa kufichua na kuzuia uhalifu kwa ajili ya polisi kata na shehia, maafisa watendaji wa kata, mitaa na vijiji.
CP Shilogire akimkabidhi DC Chikoka vitabu vya mwongozo wa kufichua na kuzuia uhalifu
Baada ya hapo, Kamishna wa Polisi Jamii, CP Shilogile, amefanya kikao na wadau mbalimbali wa Polisi Jamii ambao ni wazee wa kimila, dini, mashirika yanayosaidia watoto, wafanyabiashara, madiwani, watendaji wa vijiji, wakaguzi kata, askari kata na wananchi mbalimbali.
Ametumia kikao hicho kuelimisha wadau hao mambo mbalimbali yanayohusu Polisi Jamii, huku akiweka wazi kuwa amekutana nao ili kubadilishana mawazo ya kiutendaji kwa lengo kutokomeza uhalifu katika jamii.
Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini katika kikao hicho
Kupitia kikao hicho, wadau hao wameelimishwa pia kuhusu ukatili wa kijinsia na kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi.
Aidha, Kamishna Shilogile amewasihi wadau kujenga ujasiri wa kujitokeza kutoa taarifa za uhalifu, za huduma zinazotolewa na Jeshi la Polisi na za vitendo vya rushwa ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
CP Shilogile akisisitiza jambo katika kikao hicho
Nao wakaguzi kata walihimizwa kuelimisha wadau, ikiwa ni pamoja na elimu ya mazizi salama, usalama wetu kwanza na elimu ya ushirikishaji jamii, huku wakifanya kazi zao za kila siku kwa kufuata kaulimbiu ya Jeshi la Polisi ambayo ni “NIDHAMU, HAKI, WELEDI NA UADILIFU” katika jamii wanayoihudumia.
Katika ziara hiyo, Kamishna wa Polisi Jamii Tanzania, CP Faustine Shilogile ameongozana na SACP Mstaafu Engelbert Kiondo ambaye ni Mshauri Mkuu na Mwezeshaji Mkuu wa Polisi Jamii Tanzania, na Kamishna Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Watoto, Faidha Suleiman.
CP Shilogile (katikati mbele) katika picha ya pamoja na Maafisa wa Polisi mbele ya jengo jipya la Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kipolisi Tarime Rorya mjini Tarime, leo.
No comments:
Post a Comment