NEWS

Friday 4 August 2023

Wadau wakutana kupendekeza Wajumbe wa Kamati ya Maji Dakio la Mara



Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka (katikati mbele) katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na wadau mbalimbali wa maji na mazingira mara baada ya kufungua kikao cha kupendekeza Wajumbe wa Kamati ya Maji ya Dakio la Mara mjini Tarime, leo.
---------------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News
------------------------


WADAU wa maji na mazingira kutoka maeneo mbalimbali ya Bonde la Mto Mara wamekutana kupendekeza majina manane ya Wajumbe wa Kamati ya Pili ya Maji ya Dakio la Mara, katika kikao muhimu kilichoandaliwa na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB). 

  Akifungua kikao hicho mjini Tarime mapema leo Agosti 4, 2023, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Rorya, Juma Chikoka amewataka wadau hao kupendekeza watu wenye uwezo na waadilifu - watakaokuwa msaada kwa Dakio la Mara na LVBWB kwa ujumla. 

  “Pendekezeni majina ya watu wenye sifa watakaosaidia Dakio la Mara na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria katika juhudi za kulinda na kutunza vyanzo vya maji ili viwe endelevu kwa manufaa ya vizazi na vizazi vijanavyokuja,” amesisitiza Chikoka ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tarime.
DC Chikoka akizungumza kikaoni

  Awali, Mkurugenzi wa LVBWB, Renatus Shinhu ametaja majukumu ya Wajumbe wa Kamati ya Dakio la Mara kuwa ni kushughulikia utatuzi wa migogoro ya maji inayoweza kujitokeza, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya maji ndani ya Dakio na kutekeleza majukumu ambayo LVBWB itayakasimu kwao. 

  “Vyombo vya watumia maji vina jukumu la kuisaidia serikali katika kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinalindwa na kutunzwa pamoja na mazingira yake, hasa kwa kupanda miti,” amesema Shinhu. 
Mkurugenzi Shinhu akizungumza kikaoni

  Mkurugenzi huyo wa LVBWB ametumia nafasi hiyo pia kuzipongeza jumuiya za watumia maji mkoani Mara kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao vizuri. 

  Kikao hicho kimehudhuriwa na wadau mbalimbali wa maji na mazingira, wakiwemo kutoka jumuia za watumia maji, Halmashauri za Wilaya, Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kampuni ya Grumeti Reserves na WWF, miongoni mwa mashirika mengine yasiyo ya serikali yanayofanya kazi katika maeneo ya Bonde la Mto Mara.
Sehemu ya washiriki wa kikao hicho

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weled

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages