NEWS

Saturday 26 August 2023

Right to Play, AICT wahamasisha umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike SerengetiAfisa Mradi wa mradi wa 'Save Her Seat', Rebeca Bugota na viongozi wengine wakikabidhi kombe kwa washindi wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi katika Shule ye Msingi Wagete wilayani Serengeti jana.
------------------------------------------

Na Godfrey Marwa –
Mara Online News, Serengeti
--------------------------------------- 

SHIRIKA la Right to Play kwa kushirikiana na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe wanatekeleza mradi wa ‘Save Her Seat’ kuhamasisha wazazi na walezi wilayani Serengeti kusomesha watoto wa kike, ili waweze kutimiza ndoto zao za kielimu na maisha katika jamii. 

Akitoa elimu hiyo kupitia tamasha la michezo kwa wanafunzi lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Wagete wilayani Serengeti jana Ijumaa, Afisa Mradi wa mradi wa ‘Save Her Seat’, Rebeca Bugota alisema uwekezaji kwenye elimu ya mtoto wa kike unalipa. 

“Kuwasaidia watoto wa kike wafike kwenye mafanikio yao ni jukumu la mzazi, huwezi kuvuna mahala usipopanda - wala mazao mazuri kwenye shamba ambalo huwezi kulihudumia. Kama tunataka matokeo mazuri lazima tuwekeze kwenye elimu ya watoto wa kike sawa na wa kiume,” alisema Rebeca. 

Rebeca akitoa elimu

Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Wagete, Gideon John alikazia hoja hiyo akiwataka wakazi wa kijiji hicho kubadilika kwa kusomesha watoto wa kike ili waweze kuwa hazina ya baadaye. 

Gideon akizungumza

“Ukisomesha mtoto wa kike ni tofauti na aliyesomesha mtoto wa kiume, mtoto wa kike anaweza kuleta manufaa makubwa, hivyo tubadilike na kuelewe kuwa unapomsomesha mtoto wa kike ni hazina,” alisema Gideon. 

Naye Mchungaji Joseph Daudi wa Kanisa la Tanzania Assembles of God (TAG) la kijijini Wagete, alisema hakuna jamii inayoweza kuendelea na kuwa bora kwa kumwacha nyuma mtoto wa kike. 

“Ukimwona mwanaume mwenye mafanikio kuna mwanamke mwenye nguvu nyuma yake, hivyo watoto wa kike na wa kiume wapewe fursa sawa ya kupata elimu ili tuweze kuwa na jamii iliyo bora,” alisema Mchungaji Joseph. 
Mchungaji Joseph akizungumza

Lengo kuu la tamasha hilo la michezo ya wanafunzi chini ya mradi wa ‘Save Her Seat’ ni kuikumbusha jamii kuacha mfumo dume, mila na desturi potofu, na hivyo kumlinda na kumwezesha mtoto wa kike kupata elimu na fursa sawa na mtoto wa kiume.

Kaulimbiu ya mradi huo inasema "Elimu kwa Wasichana kwa Kesho Endelevu, Tuwalinde na Kuwapa Fursa Sawa." 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages