NEWS

Friday 25 August 2023

Right to Play, AICT wazidi kupaza sauti ya elimu kwa watoto wa kike Tarime Vijijini




Na Joseph Maunya –
Mara Online News
--------------------------- 

SHIRIKA la Right to Play limeendelea kushirikiana na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kupaza sauti ya umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike. 

Kupitia tamasha la michezo mbalimbali kwa wanafunzi wa shule za msingi Kimusi na Nyamiri zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, wanafunzi, wazazi na walezi wamehamasishwa kusaidia watoto wa kike kupata elimu. 

Mratibu wa Mradi kutoka Right to Play, Onesmo Singo akizungumza wakati wa tamasha hilo

“Tuwape watoto wa kike nafasi ya kusoma sawa na watoto wa kiume. Watoto wa kike wamekuwa wakikutana na vikwazo kama vile ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni, hivyo sote kwa pamoja tushikamane kumtetea mtoto wa kike apate elimu,” Mratibu wa Mradi kutoka Right to Play, Onesmo Singo alisema wakati wa tamasha hilo lililofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Kimusi jana. 

Kwa upande wake Kaimu Mratibu Elimu Kata ya Nyamwaga, Mwl Jacob Peter alisema “Tunasisitiza elimu kwa watoto wa kike siyo kwa sababu wao ni wa pekee, hapana, ila ni kwa sababu wao wanakumbwa na changamoto nyingi.” 

Naye Afisa Mtendaji Kijiji cha Kimusi, John Marwa Matete (anayekabidhi kombe pichani juu) aliyekuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo, alisema elimu itawezesha watoto wa kike kupata nafasi ya kufanya kazi katika ofisi za umma, kwa idadi kubwa kama ilivyo kwa wanaume. 

Mwakilishi wa timu ya wasichana akionesha kombe walilotwaa kwa ushindi

“Nimejifunza umuhimu wa sisi watoto wa kike kupata elimu, lakini pia leo tumecheza michezo mbalimbali yenye faida kubwa kwa afya zetu,” alisema Veronika Koroso Musiani, mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Nyamiri. 

Shirika la Right to Play linashirikiana na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kuendesha mradi wa kukuza ubora wa elimu kwa kuwajengea uwezo wanafunzi, walimu, wazazi na jamii kwa ujumla kupitia matamasha ya michezo kwa shule za msingi katika kata za Nyamwaga, Itiryo na Nyasincha zilizopo halmashauri ya Wilaya ya Tarime. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages