NEWS

Thursday 10 August 2023

Shirika la WWF lawakutanisha wadau kuandaa mpango kazi wa uhifadhi Dakio la Mto MaraKatibu Tawala Msaidizi wa Utawala na Rasilimali Watu Mkoa wa Mara, Dominicus Lusasi akifungua warsha ya kuandaa mpango kazi wa Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara mjini Musoma jana.
----------------------------------------------------------
Na Mwandishi wa
Mara Online News
------------------------ 

JUHUDI zaidi zinahitajika katika uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji katika Bonde la Mto Mara, kwa ustawi na uendelevu wa maisha ya binadamu, wanyama na mazingira kwa ujumla. 

Hayo yalisisitizwa na wadau katika warsha ya siku mbili ya kutathmini maendeleo ya utekelezaji na kuandaa mpango kazi wa Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara, iliyoanza jana mjini Musoma. 

Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) Tanzania, chini ya ufadhili wa Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa (USAID). “Watendaji na wenyeviti wa vijiji washirikishwe kwa karibu katika hatua za utatuzi wa matatizo yanayochangia uharibifu wa vyanzo vya maji katika bonde hili,” alisema Katibu Tawala Msaidizi wa Utawala na Rasilimali Watu Mkoa wa Mara, Dominicus Lusasi aliyekuwa mgeni rasmi katika warsha hiyo. 

Lusasi alisema uhifadhi wa Bonde la Mto Mara ambalo linajumuisha sehemu ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, ni moja ya mipango ya maendeleo ya mkoa wa Mara. Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la WWF Tanzania, Dkt Lawrence Mbwambo alisema wanaendelea kuongeza nguvu za kuisaidia Serikali katika jitihada za kutunza vyanzo vya maji katika bonde hilo. 

“Maji hayana mbadala, na maji ni muhimu kwa matumizi ya binadamu, kilimo, mifugo na wanyamapori. Hivyo tunaendelea kushirikiana na wadau, zikiwemo taasisi za Serikali katika utekelezaji wa mipango ya kuhifadhi na kutunza vyanzo vya maji na mazingira katika Bonde la Mto Mara,” alisema Dkt Mbwambo. 

Dkt Mbwambo akisisitiza jambo katika warsha hiyo

Msimamizi wa Shirika la USAID Tanzania, Mhandisi Boniphace Marwa alisema mafanikio ya utekelezaji wa mipango ya WWF, Serikali na wadau wengine katika uhifadhi na utunzaji wa Bonde la Mto Mara yatakuwa mfano wa kuigwa na mabonde mengine nchini. 

Naye Mratibu wa Miradi katika Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria kutoka nchi ya Kenya, Mhandisi Hilda Luoka alisema mto Mara ni chanzo muhimu cha ziwa hilo la kimataifa, hivyo unastahili kutunzwa kwa nguvu zote za hali na mali kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo. 

Awali, Mratibu wa miradi ya maji wa WWF Tanzania, Mhandisi Christian Chonya alisema Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara ni wa miaka mitatu, ulianza Aprili 2022 na utakamilika Aprili 2025.

Mhandisi Chonya akiwasilisha maelezo ya mradi huo

Washiriki wengine wa warsha hiyo ni kutoka Wizara ya Maji, halmashauri za wilaya, mashirika yasiyo ya Serikali ya uhifadhi wa mazingira, na jumuiya za watumia maji kutoka wilaya sita zinazounda mkoa wa Mara; ambazo ni Serengeti, Butiama, Tarime, Rorya, Musoma na Bunda. 

Washiriki wa warsha hiyo wakiwa katika picha ya pamoja

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages