
Rais Samia Suluhu Hassan akilihutubia Bunge la 13 jijini Dodoma, Novemba 14, 2025.
Akiripoti kutoka
Dodoma
------------

Awasamehe waliokamatwa

Kuunda Tume ya Maridhiano
“Tanzania ina demokrasia iliyokomaa, hata hivyo tutaendelea kuiboresha kulingana na mazingira na wakati. Ni jukumu letu sasa kujielekeza kwenye maboresho hayo kwa utashi wetu bila shinikizo lolote,” alisema Rais Samia.
Dodoma
------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameongoza wabunge na wageni waalikwa kuomboleza na kuwaombea watu waliopoteza maisha katika vurugu zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 29, 2025.
“Nimehuzunishwa sana na tukio lile. Natoa pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao, na tunamuomba Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani.
“Majeruhi tunawaombea wapone kwa haraka, na kwa wale waliopoteza mali zao tunawaomba wawe na stahamala na uvumilivu,” alisema Rais Samia wakati alipokwenda kuzindua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma jana Novemba 14, 2025.

Awasamehe waliokamatwa
Aidha, Rais Samia aliagiza kuwachiwa kwa watu waliokamatwa na kufunguliwa kesi za uhaini, hususan waliojiingiza kwenye vurugu na uvunjifu wa amani kwa kufuata mkumbo.
“Ninatambua kwamba vijana wengi waliokamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini hawakujua wanachokifanya. Nikiwa Mama na Mlezi wa Taifa hili, ninavielekeza vyombo vya sheria na hasa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana wetu,” alisema na kuendelea:
“Kwa wale ambao wanaonekana walifuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu wawafutie makosa yao. Ninatoa msamaha huo kwa sababu, hata maneno ya Mungu katika Kitabu cha Luka sura ya 23 Mstari wa 34 yanasema, na hapa nanukuu: “Yesu akasema, Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo.”
Katika hotuba yake, Rais Samia pia aliwasihi vijana kuongozwa na dhamira ya maelewano na kujirekebisha, wa kitambua kwamba nchi yao imejengwa kwenye misingi ya amani na utulivu wa kisiasa.
“Sisi wazazi wenu tungeshawishika kuyafanya mliyoyafanya wakati huu, nchi hii isingekuwa na neema na maendeleo mnayoyaona leo. Niwasihi sana wanangu, nchi hii ni yenu, kwa shida zozote zile zinazowakabili, msikubali hata siku moja kushawishiwa kuichoma nchi yenu wenyewe.
“Msikubali kukata tawi la mti ambalo mmelikalia. Hili nawaomba mlikatae kwa nguvu zenu zote. Ninyi ndio walinzi na wajenzi wa Taifa hili, nawasihi kamwe msije kuwa Wabomoaji wa Taifa lenu,” alisisitiza Rais Samia.
Hata hivyo, Rais alisema serikali imechukua hatua ya kuunda Tume ya kuchunguza machafuko yaliyotokea ili kujua kiini chake. “Taarifa hiyo [ya uchunguzi huo] itatuongoza kujielekeza kwenye mazungumzo ya kuleta maelewano na amani,” alisema.

Kuunda Tume ya Maridhiano
Sambamba na hayo, Rais Samia aliahidi kuunda Tume ya kuanzisha Mazungumzo ya Maridhiano na Upatanishi na kuandaa mazingira ya kuanza kwa Mchakato wa mabadiliko ya Katiba - kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025-2030.
“Katika muhula kwa kwanza wa Awamu ya sita tulikuja na falsafa ya R4 ili kuliunganisha Taifa. Serikali ilionesha utayari wakati wote kuleta maridhiano, ili kwa pamoja tuweze kulijenga na kulitunza Taifa letu. Serikali ilinyoosha mkono kuwavuta na kuwakaribisha vyama vya siasa, vyama vya kijamii, sekta binafsi na hata Jumuiya za Kimataifa, ili kwa pamoja tuijenge Tanzania.
“Mkono huo wa urahimu ulileta matumaini kwa nchi, kabla ya baadhi ya wadau kuamua kuuachilia. Kwa kuwa wananchi wa Tanzania wamenipa ridhaa ya kuendelea kuiongoza nchi hii, sitachoka kunyoosha tena mkono wa maridhiano.
“Ni matumaini yangu kuwa wadau wa kisiasa wataupokea kwa dhati mkono wa maelewano, ili kwa pamoja tujenge mazingira muafaka kwa maendeleo ya Taifa letu. Tutajifunza kutokana na makosa na mapungufu ya taasisi zetu za kidemokrasia.
“Tanzania ina demokrasia iliyokomaa, hata hivyo tutaendelea kuiboresha kulingana na mazingira na wakati. Ni jukumu letu sasa kujielekeza kwenye maboresho hayo kwa utashi wetu bila shinikizo lolote,” alisema Rais Samia.
No comments:
Post a Comment