NEWS

Sunday 20 August 2023

Twiga Minerals yang’ara ubia na Serikali, yatoa gawio la shilingi bilioni 84



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan akikabidhi Tuzo ya Ushindi wa Kampuni ya Twiga Minerals katika utoaji gawio wa kampuni hiyo yenye ubia na Serikali.
-----------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
---------------------------
 

KAMPUNI ya Twiga Minerals Cooperation Limited inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick Gold Cooperation, imeongoza katika kipengele cha kampuni zenye ubia na Serikali katika utoaji gawio. 

Tuzo ya ushindi kwa kampuni hiyo ilitolewa jana Agosti 19, 2023 jijini Arusha na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu na Taasisi za Umma, kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Jukwaa la Wakuu wa Taasisi za Umma. 

Akizitaja kampuni zilizofanya vizuri katika kipengele hicho, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu alisema Kampuni ya Twiga imefanya vizuri kwa kuipatia Serikali gawio la kiasi cha shilingi bilioni 84 katika mwaka wa fedha 2022/23. 

Kampuni ya Barrick ndiyo ya kwanza kuingia ubia na Serikali miongoni mwa kampuni za madini, hali ambayo ilihamasisha na nyingine kutoka nje kusaini na Serikali mikataba yenye thamani kubwa katika shughuli za uchimbaji wa madini ya aina mbalimbali, yakiwemo madini muhimu na ya mkakati. 

Aidha, ubia na kampuni hiyo umetajwa mara kadhaa kuwa mfano wa kuigwa na mataifa mbalimbali, huku ikitaja kuutumia ubia wa Tanzania na kuutekeleza katika nchi nyingine ilikowekeza. 

Migodi iliyo chini ya Kampuni ya Twiga Minerals ni pamoja na North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi. 

Januari 2023, wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Barrick nchini Tanzania, Melkiory Ngido alisema mwaka 2020 kampuni hiyo iliipatia Serikali gawio kiasi cha Dola za Marekani milioni 250, huku kipindi cha mwaka 2017 hadi 2022 kiasi cha shilingi bilioni 24.3 kilitolewa kwa ajili ya halmashauri kama tozo mbalimbali katika maeneo yenye shughuli za migodi yake. 

“Kampuni ya Twiga imepanga kuendeleza shughuli za utafiti ili kuongeza uhai wa migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu, ambapo matazamio ya uhai wa mgodi wa Bulyanhulu ni kufika mwaka 2040 na North Mara ni kufika mwaka 2039,” alisema Ngido katika kikao hicho.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages