Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele (mwenye kipaza sauti) akimmkabidhi mmoja wa walimu kwa niaba ya wenzake wa Shule ya Sekondari Tarime cheti cha pongezi kufuatia ufaulu mzuri wa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita shuleni.
-----------------------------------------------------------
Na Joseph Maunya – Mara Online News, Tarime
------------------------------------
WALIMU wa Shule ya Sekondari Tarime mkoani Mara wamesherehekea na kupongezwa kufuatia matokeo mazuri ya wanafunzi wao waliohitimu kidato cha sita mwaka huu wa 2023.
Aidha, walimu hao wametunukiwa vyeti na shilingi milioni 10 wakati wa hafla iliyofanyika shuleni hapo leo Agosti 24, ambayo iliyoandaliwa na uongozi wa shule hiyo kuwapongeza, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele.
DC Mntenjele akizungumza katika hafla hiyo
“Niwapongeze walimu wote kwa juhudi zenu mlizoonesha mpaka kufanikisha jambo hili, nawapongeza pia wanafunzi waliomaliza, na ninyi watarajiwa mjiandae mapema ili mwezi wa tano mwakani muwe tayari kwa mitihani.
“Lakini pia walimu mkumbuke kujiendeleza kitaaluma mkiwa kazini kwa ajili ya kupata fursa nyingine siku za usoni, maana hujui ni wakati gani atahitajika mtu mwenye elimu kubwa zaidi, hivyo ukisoma mapema unakuwa tayari wakati wowote,” amesema DC Mntenjele.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo amesema “Tarime Sekondari mmebeba jina la halmashauri yetu na wilaya nzima, mkifaulu siyo ninyi tu, pia mnatuheshimisha mpaka sisi viongozi, hivyo wanafunzi msome kwa bidii.”
TD Gimbana Ntavyo akizungumza katika hafla hiyo
Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule hiyo, Mwl Maro Chenge, kati ya wanafunzi 498 waolifanya mtihani wa Taifa wa kuhitimu Kidato cha Sita mwaka huu(2023), 357 wamepata ufaulu wa daraja la kwanza, 130 daraja la pili, 11 daraja la tatu na hakuna daraja la nne wala sifuri.
Mwl Chenge akizungumza kwa furaha katika hafla hiyo
Hafla hiyo ya kuwapongeza walimu na wanafunzi hao pia ilihudhuriwa na viongozi wengine mbalimbali wakiwemo wa elimu, kisiasa, kidini, walimu na wazazi wilayani Tarime.
No comments:
Post a Comment