Na Mwandishi Wetu –
Mara Online News, Bunda
------------------------------------
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
Mara Online News, Bunda
------------------------------------
MAHAKAMA ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara imewatia hatiani watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa mashtaka ya uhujumu uchumi.
Mtumishi wa kwanza ni Emmanuel Jeremiah aliyekuwa mkusanya mapato ya halmashauri kwa njia ya POS, ambaye ametiwa hatiani kwa ufujaji wa shilingi 9,644,065, hivyo kuhukumiwa kwenda jela miaka miwili, au kulipa faini ya shilingi 200,000 na kurejesha fedha hizo za halmashauri.
Mwingine ni Afisa Kilimo, Fikiri John Tendw ambaye pia alikuwa mkusanya mapato ya halmashauri kwa njia ya POS, aliyetiwa hatiani kwa ufujaji wa shilingi 4,163,165, hivyo naye amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani, au kulipa faini ya shilingi 200,000 na kurudisha fedha hizo za halmashauri.
Hukumu hizo zilitolewa hivi karibuni na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya Bunda, Betron Costantine Sokanya, ambaye alisema Jamhuri imethibitisha kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo ya uhujumu uchumi.
Mashauri hayo yalifunguliwa na kuendeshwa na Wakili Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mwinyi Yahaya.
Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na makosa hayo chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Mapitio ya Mwaka 2022 na Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Mapitio ya Mwaka 2022.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment