NEWS

Friday 25 August 2023

Wenyeviti wa mitaa kuanza kushirikikishwa vikao vya madiwani Tarime Mji



Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo mjini Tarime leo Ijumaa.
-----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu –
Mara Online News
----------------------------- 


WENYEVITI na watendaji wa mitaa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara, wataanza kushirikishwa kwenye vikao vya baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, kwa ajili ya kutoa taarifa za maendeleo ya maeneo yao ya uongozi. 

Msimamo huo umetangazwa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Daniel Komote mjini Tarime leo Ijumaa katika kikao cha baraza la madiwani hao, kilichojadili taarifa za maendeleo ya kata zao kwa kipindi cha Aprili - Juni 2023. 

Madiwani kikaoni

“Pia tunataka tuwe na utaratibu wa kuwaita wananchi wa kata zetu kwenye vikao vyetu vya baraza la madiwani ili wajifunze na kupata uelewa kwa kajili ya kutusaidia kuhamasisha maendeleo,” ameongeza Komote ambaye ameonesha mfano kwa kuwakaribisha katika kikao hicho viongozi wa mitaa na baadhi ya wananchi kutoka kata yake ya Nkende. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo amewakumbusha maafisa watendaji wa kata kuhakikisha maeneo ya umma yanatengwa katika kata zao kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayojitokeza. 

Mkurugenzi Gimbana akizungumza katika kikao hicho

“Endeleeni kutenga maeneo kwa ajili ya miradi, hasa ya afya na elimu ili kuepuka kukosa fursa za kujengewa huduma hizo kwa ajili ya wananchi wa kata zenu,” Gimbana amesisitiza na kuwaelekeza watendaji hao kuhakikisha pia maeneo ya umma yaliyovamiwa kwenye kata zao yanarejeshwa. 

Katika hatua nyingine, madiwani hao wamemchagua kwa mara nyingine tena Diwani wa Kata ya Nyamisangura, Thobias Ghati kuendelea na nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo. 

Awali, baraza la madiwani hao limewakaribisha kikaoni walimu wa Shule ya Sekondari Tarime kuwapongeza na kuwatunuku vyeti maalum kutokana na ufaulu mzuri wa wanafunzi wao katika Mtihani wa Taifa wa kuhitimu Kidato cha Sita mwaka huu wa 2023. 

Mkuu wa Shule ya Sekondari Tarime, Mwl Maro Chenge (kushoto mbele) na walimu wenzake wakijitambulisha katika kikao hicho cha Baraza la Madiwani.


Mwenyekiti Komote akimkabidhi mwalimu acheti cha pongezi

Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule hiyo, Mwl Maro Chenge, kati ya wanafunzi 498 waolifanya mtihani wa Taifa wa kuhitimu Kidato cha Sita mwaka huu, 357 wamepata ufaulu wa daraja la kwanza, 130 daraja la pili, 11 daraja la tatu na hakuna daraja la nne wala sifuri. 

Kikao hicho cha Baraza la Madiwani kimehudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl Saul Mwaisenye, miongoni mwa viongozi na wataalamu wengine. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages