NEWS

Thursday 21 September 2023

Kamati ya Siasa CCM yakagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo Halmashauri za Tarime Mji na Vijijini



Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho (kushoto) akiongoza wajumbe wengine kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la utawala katika Shule ya Sekondari mpya Gicheri jana Jumatano.
-------------------------------------------------

Na Joseph Maunya, Tarime –
Mara Online News
-----------------------------


KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara, imefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ya elimu katika Halmashauri za Mji wa Tarime na Tarime Vijijini. 

Ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Marwa Daudi Ngicho, Kamati hiyo jana ilikagua ujenzi wa Shule ya Sekondari mpya Gicheri, miongoni mwa miongoni mwa miradi mingine. 

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa jengo la utawala la Shule ya Sekondari Gicheri, Ngicho alisema kukamilika kwa shule hiyo kutasaidia kupunguza adha ya msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Nkende.


Mwenyekiti Ngicho (kushoto) akizungumza wakati wa ukaguzi wa jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Gicheri. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo.

“Kamati ya Siasa imekuja kukagua hii shule, tumejiridhisha kwamba kazi inaendelea, tunachowasihi mkamilishe hili jengo kwa wakati ili muweze kuomba usajili na mwakani shule ichukue watoto waanze kusoma, na hilo ndilo lengo la Serikali yetu. 

“Nampongeza Mheshimiwa Rais [Samia Suluhu Hassan] kwa kuleta pesa, na vile vile Mkurugenzi [Gimbana Ntavyo] kwa kutenga mapato ya ndani kwa ajili ya kukamilisha jengo hili, tunaomba mfanye hii kazi kwa speed (kasi) na watoto mwakani waingie kwenye hii shule,” alisema Ngicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime.


Jengo la utawala linaloelekea kukamilishwa katika Shule ya Sekondari Gicheri

Awali, akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa jengo hilo la utawala shuleni hapo, mwakilishi wa mhandisi anayesimamia mradi huo alisema Halmashauri ya Mji wa Tarime tayari imetoa fedha kiasi cha shilingi milioni 37 za mapato ya ndani ili kumalizia ujenzi huo. 


Sehemu ya vyumba vya madarasa vya Shule ya Sekondari Gicheri

Miradi mingine iliyotembelewa na Kamati hiyo ya Siasa ya CCM Wilaya ya Tarime ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Msingi Kemwita iliyopo kata ya Nkende, ujenzi wa Soko Kuu la Tarime, miongoni mwa mingine katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Tarime Mji. 

Kamati hiyo inaendelea na ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo leo Alhamisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime [Vijijini], ambapo mapema leo asubuhi tayari imeshakagua miradi kadhaa ikiwemo ya BOOST katika eneo la Nyamongo na kata ya Kwihancha.

Ukaguzi ukiendelea kwenye mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kwihancha.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages