NEWS

Thursday 21 September 2023

Magoto FC yatwaa ubingwa mashindano ya Kiles Cup, Mbunge Waitara aongeza zawadi



Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara akikabidhi kombe kwa timu ya Magoto FC iliyotwaa ubingwa wa mashindano ya Kiles Cup jana. Mwenye kodi la kijivu ni Diwani wa Kata ya Nyakonga, Simion Kiles Samwel aliyedhamini mashindano hayo.
--------------------------------------------

Na Joseph Maunya, Tarime –
Mara Onlin News
---------------------------


MASHINDANO ya soka ya Kiles Cup yamehitimishwa kwa Timu ya Magoto FC kutwaa ubingwa, baada ya kuichapa Nyakonga FC bao 1-0, katika mechi ya fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Magoto, jana Jumatano. 

Mashindano hayo yamedhaminiwa na Diwani wa Kata ya Nyakonga, Simion Kiles Samwel ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. 



Awali, zawadi za washindi wa mashindano hayo zilipangwa kuwa ni kombe, shilingi laki tatu na mpira kwa mshindi wa kwanza, shilingi laki moja na nusu na mpira kwa mshindi wa pili na shilingi laki moja na mpira kwa mshindi wa tatu. 

Hata hivyo, mgeni rasmi wa fainali hiyo, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara aliunga mkono juhudi hizo za Diwani Kiles kwa kuongeza shilingi laki moja na mpira kwa kila mshindi. 

Kwa upande wake Diwani Kiles alisema lengo la kuanzisha mashindano hayo ni kupata timu ya kata ya Nyakonga itakayochuana na timu ya Sekondari, lakini pia timu za kata nyingine. 

“Tunashukuru Mungu tumecheza na kumaliza salama, lakini pia tunamshukuru Mheshimiwa Kiles kudhamini mashindano haya,” alisema Mwita Senso, mfungaji wa bao pekee la ushindi wa timu ya Magoto FC. 

Mashindano hayo ya Kiles Cup yalizishirikisha timu tatu za Nyakonga, Kebweye na Magoto, ambapo yamewapa vijana wa kata ya Nyakonga fursa ya kuonesha vipaji vyao pamoja na kuunda timu ya kata kwa ajili ya mashindano mengine ndani ya jimbo la Tarime Vijijini. 

Awali, akizindua mashindano hayo hivi karibuni, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Noverty Kibaji alimpongeza Diwani Kiles kwa kutekeleza agizo la chama hicho tawala. 

“Tuliagiza sisi kamati ya Siasa ya Wilaya kwamba waheshimiwa madiwani wasimamie na kutekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi kwa kufufua michezo katika kata zote. Mwaka 2024 na 2025 kupitia michezo tuna hakika tutawapata vijana watakaopiga kura kwa CCM wenye afya njema,” alisema Kibaji. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages