NEWS

Monday 11 September 2023

Mbunge Waitara aridhishwa na ushirikiano wa mgodi wa Barrick North Mara kwa kampuni za wazawa, aipongeza Kemanyanki kuwajali vijanaMbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara akizungumza wakati wa fainali ya mashindano ya soka ya Kemanyanki Cup kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe mjini Nyamongo jana Jumapili.
----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu –
Mara Online News
---------------------------


MBUNGE wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara ameeleza kuridhishwa na ushirikiano unaooneshwa na Kampuni ya Barrick kwa kampuni za wazawa na jamii inayozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara. 

Pia ameonesha kuridhishwa na jitihada za kujali kundi la vijana zinazofanywa na kampuni ya kizalendo ya Kemanyanki ambayo inafanya kazi na mgodi huo uliopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara. 

Waitara aliyasema hayo wakati wa fainali ya mashindano ya soka ya Kemanyanki Cup yaliyoandaliwa na kampuni hiyo ya kizalendo, yakizishirikisha timu 12 za vijana kutoka vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo. 

Mechi ya fainali ya mashindano hayo - kati ya Kewanja FC na Mrito FC ilichezwa katika uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe iliyopo mjini Nyamongo jana Jumapili. 


Timu zikichuana uwanjani

“Ninawapongeza vijana waliounda kampuni ya kizalendo ya Kemanyanki kwa kuamua kukileta kidogo walichonacho kwenye jamii. Lakini pia niwapongeze mgodi wa North Mara kwa ushirikiano wao wa kila mara, haya ndiyo tunayotaka yaendelee kufanyika,” alisema Mbunge Waitara ambaye alikuwa mgeni rasmi katika fainali hiyo. 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kemanyanki, Nicolaus Mgaya aliishukuru kampuni ya Barrick kwa kuona umuhimu wa kufanya kazi na kampuni za wazawa katika mgodi wa North Mara. 

Mgaya alisema wananchi wanaoishi vijiji vinavyozunguka mgodi huo wana kila sababu ya kujivunia uwepo wa Kampuni ya Kemanyanki na mgodi huo kutokana na kuwatengenezea fursa za ajira na biashara. 

Akizungumzia mashindano ya Kemanyaki Cup, Mgaya alisema yamewezesha vijana kuufahamu vizuri mgodi wa North Mara na faida zake kwa umma, lakini pia wameweza kubadilishana mawazo yenye manufaa katika maisha yao na jamii inayozunguka mgodi huo. 


Mkurugenzi Mtendaji wa Kemanyanki Cup, Nicolaus Mgaya akizungumza wakati wa fainali hiyo.

“Kemanyanki ni kampuni ya jamii ya vijiji vinavyozunguka mgodi, unapoiona Kemanyanki popote pale ujue ni mali yako,” alisema Mgaya na kuendelea: 

“Tunataka kuibua vipaji ndani ya jamii, kudumisha ushirikiano, kutengeneza network (mtandao) katika jamii yetu na kutumia vizuri fursa zilizopo. Tunahitaji vijana wetu wawe ndio sehemu kubwa ya kuifaidi keki tunayoipata.” 

Katika mchezo wa fainali ya Kemanyanki Cup uliokuwa na ushindani mkali, Kewanja FC iliibuka mshindi kwa kuichapa Mrito FC kwa mikwaju ya penati 4-2. 

Kwa ushindi huo Kewanja ilitwaa kombe, medali, jezi na shilingi 800,000 huku Mrito ikipata jezi, medali na shilingi 450,000 na Nyangoto iliyoshika nafasi ya tatu ilipata medali, jezi na shilingi 300,000, shukrani kwa Kampuni ya Kemanyanki. 


Afisa Rasilimali Watu wa Kampuni ya Kemanyanki, Celina Mkaro akisoma taarifa ya mashindano hayo.

Kemanyanki ni moja ya kampuni za wazawa zinazofanya kazi na Kampuni ya Barrick katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kutoa huduma mbalimbali. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages