NEWS

Thursday 14 September 2023

Mwanaume anaedaiwa kumdhalilisha mwandishi wa habari wa kike akitangaza kipindi nchini Uhispania atiwa mbaroni




POLISI nchini Uhispania wamemkamata mwanaume anayetuhumiwa kumnyanyasa kingono mwandishi wa habari wa kike, baada ya kudaiwa kumgusa makalio alipokuwa akitangaza kipindi mbashara kwenye TV.

Isa Balado alikuwa akiripoti kuhusu wizi wa mjini Madrid siku ya Jumanne wakati mwanaume huyo alipojitokeza na kuonekana kumgusa makalio. 

Balado alijaribu kuendelea, lakini alikatizwa na mtangazaji wa kipindi hicho. "Isa, nisamehe kwa kukukatisha... lakini alikugusa tu makalio?" Nacho Abad aliuliza. 

Mwandishi huyo alithibitisha hilo, na Abad akamwambia amuweke "mpumbavu" huyo kwenye kamera ili kuwaonesha Isa Balado na mwanaume huyo, ambaye bado alikuwa amesimama naye, akitabasamu na kucheka. 

"Kama unavyotaka kuuliza tunatoka chaneli gani, ni lazima uniguse makalio kabisa? Ninafanya kipindi cha moja kwa moja na ninafanya kazi," Balado alimwambia. 

Polisi baadaye walisema mwanaume mmoja alikamatwa kwa madai ya kumpiga mwandishi wa habari alipokuwa akifanya kipindi cha televisheni, katika ujumbe uliotumwa kwenye X, zamani Twitter. 

Mediaset Espana, inayomiliki kituo cha habari, ilitoa taarifa ikieleza kumuunga mkono Balado baada ya "hali isiyovumilika kabisa" aliyokumbana nayo, na kwamba "inakataa kabisa aina yoyote ya unyanyasaji au uchokozi". 

Waziri wa Kazi wa Uhispania, Yolanda Díaz pia alizungumza tukio hilo. Aliandika kwenye X: "Ni matukio ambayo huwafanya waandishi wa habari kuteseka na unyanyasaji wa kijinsia kama huu, na wachokozi ni watu wasiotubu mbele ya kamera." 

Tukio hili linakuja huku kukiwa na mzozo wa ubaguzi wa kijinsia nchini Uhispania, uliochochewa na rais wa zamani wa FA wa nchi hiyo, Luis Rubiales akimbusu mshindi wa Kombe la Dunia, Jenni Hermoso kwenye midomo. 

Vitendo vyake wakati wa Fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake vilisababisha kukosolewa na watu wengi, hatimaye kujiuzulu na kuitwa mahakamani kwa tuhuma za unyanyasaji wa kingono na kulazimisha. BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages