NEWS

Friday 15 September 2023

Siku ya Mto Mara 2023: Serikali yaipongeza Barrick kwa kushiriki uboreshaji huduma ya maji, utunzaji mazingira




Na Mwandishi Wetu, Serengeti –
Mara Online News
--------------------------- 


NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi ameipongeza Kampuni ya Barrick kwa kuiunga mkono Wizara ya Maji na Serikali kwa ujumla katika uboreshaji huduma ya maji kwa wananchi, kutunza mazingira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania. 

“Hongereni sana Barrick kwa shughuli mnazofanya kusaidiana na Wizara ya Maji na Serikali kwa ujumla katika uboreshaji wa huduma ya maji kwa wananchi, lakini pia utunzaji wa mazingira na kuinua uchumi wa nchi yetu,” amesema. 

Mhandisi Mahudi ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la Barrick wakati wa kilele cha Maadhimisho ya 12 ya Siku ya Mto Mara yaliyofanyika kwenye uwanja wa Sokoine uliopo mjini Mugumu katika wilaya ya Serengeti, mkoani Mara leo Ijumaa. 


Naibu Waziri Mahundi (wa pili kushoto) na viongozi wengine wakisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Mazingira wa Barrick North Mara, Samwel Ingram alipotembelea banda la kampuni hiyo.

Kampuni ya Barrick imeshiriki maadhimisho hayo kupitia Mgodi wake wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara. 

Hata hivyo, Mhandisi Mahundi ameihimiza Barrick North Mara kuendelea kuhakikisha shughuli zake za uchimbaji madini hazisababishi uchafuzi wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla katika jamii inayozunguka mgodi huo. 


Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Makungu Msalika ni miongoni mwa wageni waliotembelea banda la Barrick North Mara katika maadhimisho haya.

Awali, Afisa Mazingira wa Mgodi wa Barrick North Mara, Samwel Ingram amemweleza Naibu Waziri Mahundi kuwa shughuli za mgodi huo zinafanyika katika eneo lililo ndani ya Bonde la Mto Mara, hivyo wanawajibika kulinda usalama wa vyanzo vya maji na mazingira yanayouzunguka. 

Kuhusu huduma ya maji, Ingram amesema wanazingatia viwango vinavyokubalika kisheria katika kuchukua maji ya Mto Mara na kuyatibu kwa ajili ya matumizi ya ndani ya mgodi na kuyasambaza kwa wananchi wa vijiji vinavyopakana nao. 

“Kwa upande mwingine, Barrick North Mara tunashirikiana na Serikali kupitia mamlaka husika zikiwemo Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijiji (RUWASA) na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) kuboresha huduma ya maji na utunzaji wa mazingira. 

“Pia tunashiriki kwa vitendo kuiunga mkono Serikali katika juhudi za upandaji wa miti ili kutunza mazingira, sambamba na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi na kutunza vyanzo vya maji na mazingira,” amesema Afisa Mazingira huyo wa Barrick North Mara. 


Wenyeviti wa Halmashauri; Daniel Komote (kulia) wa Tarime Mji na Simion Kiles wa Tarime DC wakisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Maendeleo ya Jamii wa Barrick North Mara, Safarani Msuya walipotembelea banda la kampuni hiyo wakati wa maadhimisho hayo.

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mto Mara hufanyika Septemba 15 kila mwaka, ambapo nchi za Tanzania na Kenya zinazoshirikiana kuyaadhimisha hupokezana kuyaandaa kwa lengo la kuhamasisha uhifadhi na utunzaji endelevu wa Mto Mara ambao unatiririsha maji katika Ziwa Victoria. 

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya 12 ya Siku ya Mto Mara mwaka huu wa 2023 inasema “Hifadhi Mto Mara kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi endelevu”. 

Kikundi cha sanaa kutoka Kenya kikitumbuiza wakati wa kilele cha Maadhimisho ya 12 ya Siku ya Mto Mara mjini Mugumu wilayani Serengeti, Mara - Tanzania.

#Tunakuhabarisha Uweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages