NEWS

Thursday 28 September 2023

Mwera Jazz Band yanogesha tamasha la uzinduzi wa Kampeni ya Ongea Nao Festival 2023Mwera Jazz Band ikitumbuiza kwenye tamasha la uzinduzi wa Kampeni ya Ongea Nao Festival 2023 lililoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya wiki iliyopita.
----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
--------------------------------------- 


JESHI la Polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya limeandaa na kuzindua Kampeni ya Ongea Nao Festival 2023, huku Mwera Jazz Band kutoka Professor Mwera Foundation ikitumbuiza na kuwa kivutio cha aina yake katika uzinduzi huo. 

Tamasha la uzinduzi wa kampeni hiyo lilifanyika wiki iliyopita katika uwanja wa Kanisa Katoliki Komaswa wilayani Rorya, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, Juma Chikoka. 

Mbali na Mwera Jazz Band uzinduzi huo ulipambwa pia na michezo mbalimbali ikiwemo rede, kufukuza kuku, kukimbia na magunia, mpira wa miguu na kuvuta kamba. 


Kampeni hiyo ya Ongea Nao Festival 2023, ilianzishwa kwa juhudi za Jeshi la Polisi kupitia Kamisheni ya Ushirikishaji Jamii, na kuzinduliwa Kitaifa mkoani Dodoma, Juni 2023, ikiwa na lengo la kuelimisha jamii juu ya kubaini, kuzuia na na kutanzua uhalifu wa aina mbalimbali, ukiwemo ukatili wa kijinsia na unyanyasaji watoto. 

Katika hotuba yake, DC Chikoka aliwataka wananchi kujiepusha na vitendo vya uhalifu na ukatili katika Mkoa wa Polisi Tarime Rorya. 

“Naomba nichukue nafasi hii kuwataka wananchi wenye tabia ya kufanya vitendo vya uhalifu ikiwa ni pamoja na ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto kuacha mara moja, na pindi yanapotokea mtoe taarifa kwa Jeshi la Polisi wahalifu wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema. 

Hata hivyo, DC Chikoka alitumia nafasi hiyo pia kuwapongeza wadau wa maendeleo kutoka mashirika binafsi na idara za serikali waliotunukiwa vyeti kutokana na mchango wao mkubwa kwa Jeshi la Polisi Tarime Rorya katika kuunga mkono jitihada za kuzuia uhalifu wa aina zote. 

“Hii iwe chachu kwa jamii nzima kuungana na kushirikiana na Jeshi la Polisi kupinga vitendo vya uhalifu,” alisema. 
Mapema wadau mbalimbali waliohudhuria tamasha hilo la uzinduzi wa Kampeni ya Ongea Nao Festival 2023, walianza kwa maandamano ya amani yaliyoongozwa na wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo. 

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages