NEWS

Tuesday 12 September 2023

Rais Samia ateuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushauri kuhusu Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi DunianiRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan.
---------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
-----------------------------

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ameteuliwa rasmi kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kituo cha Dunia cha Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi (Advisory Board of the Global Centre on Adaptation - GCA). 

Taarifa ya uteuzi huo iliwasilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya GCA na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alipokutana na Rais Samia pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika Nairobi, Kenya hivi karibuni. 

Heshima hii ni utambuzi wa uongozi mahiri wa Rais Samia katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Afrika na duniani, ambapo Tanzania ni kinara kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali barani Afrika. 

Wajumbe wengine wa Bodi hiyo ni Rais wa Jamhuri ya Senegal, Macky Sall, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Akinumwi Adesina na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF), Kristalina Georgieva. 

GCA ni taasisi kubwa duniani inayosimamia masuala ya uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, ambapo hadi sasa imeweza kufanikisha upatikanaji Dola za Marekani zaidi ya bilioni 50. 

Tanzania inatajwa kuwa ni miongoni mwa nchi za kwanza zitakazonufaika na fedha hizo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages