NEWS

Monday 18 September 2023

RC Mtanda azuru Nyanungu, akagua vigingi vya mpaka wa hifadhi, azungumza na wanavijiji



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kijijini Kegonga juzi.
---------------------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu, Tarime
------------------------------------------- 

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda amefanya ziara ya kikazi katika kata ya Nyanungu wilayani Tarime na kukagua vigingi vilivyowekwa na Serikali kutengenisha mpaka wa Hifadhi ya Taifa Serengeti na vijiji vya kata hiyo. 

Baada ya kukagua vigingi hivyo katika kijiji cha Kegonga juzi, RC Mtanda alifanya mkutano wa hadhara na wakazi wa kijiji hicho. 

“Tumefurahi RC ametutembelea na tumeongea naye vizuri. Ametembelea eneo la bikoni (vigingi) na sisi maombi yetu ni mashamba,” Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kegonga, Waryoba Mogoyo alilimabia gazeti hili mara baada ya mkutano huo. 

Mogoyo alisema wananchi tayari wamelima na kupanda mazao katika sehemu ya eneo lililoingia ndani ya hifadhi baada ya uwekaji wa vigingi hivyo miezi michache iliyopita. 

Alitaja vitongoji vya kijijini kwake vyenye wananchi ambao mashamba yao yamepitiwa na vigingi hivyo kuwa ni Gyema, Kwibate, Borasa na Isorya. 

“Sisi tumeshapanda mahindi na ulezi, na wakati tukisubiri tamko la Serikali, maombi ya wananchi ni mashamba yarudi. Kuhusu mifugo wameshatuahidi kutuchimbia malambo,” alisema. 

Mbali na kijiji cha Kegonga, vigingi hivyo viliwekwa pia katika kijiji jirani cha Nyandage katani Nyanungu na baadhi ya vijiji vya kata za Kwihancha na Gorong’a. 

Katika ziara hiyo, RC Mtanda aliambatana na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara na Diwani wa Kata ya Nyanungu, Tiboche Richard. 

Mkuu huyo wa mkoa alisisitiza umuhimu wa mazungumzo kati ya Serikali na wananchi ambao mashamba yao yamepitiwa na vigingi hivyo. 

“Tukikaa Serikali na wahusika ndio tutajua way forward (namna ya kwenda) ili tusiendelee kugombana, ndicho kimenileta hapa. Waathirika wenyewe ndio wanapaswa kukaa na Serikali,” alisisitiza RC Mtanda. 

Alisema alizuru eneo hilo kuona changamoto zilizojitokeza baada ya uwekaji wa vigingi ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi. 

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages