
Na Mwandishi Wetu
Mahakama ya Rufani Tanzania imetupilia mbali zuio la kutofanya shughuli za kisiasa lililokuwa limewekwa na Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Uamuzi huo wa kukiweka huru CHADEMA na kukiruhusu kuendelea na shughuli zake za kisiasa ulitolewa Aprili 15, 2026 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Jaji Augustine Mwarija, Jaji Issa Maige na Jaji Abraham Mwampashi.
Uamuzi huo umetokana na mashauri ya mapitio ya mahakama yaliyofunguliwa na mahakama kutokana na kesi ya msingi ya madai ya mgawanyo usiyo sawa wa rasilimali za chama hicho baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Kesi hiyo ilifunguliwa Mahakama Kuu Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CHADEMA, Said Issa Mohamed na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini ya chama hicho kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Walalamikiwa katika kesi hiyo walikuwa Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa CHADEMA na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Mara baada ya kutolewa kifungoni, CHADEMA kimetangaza kufungua tena ofisi zake kote nchini, ikiwa ni takriban mwaka mmoja tangu kuzuiwa kujihusisha na masuala ya siasa.
Viongozi wa CHADEMA waitaja hatua hiyo ya kuondolewa kifungoji kama nuru iliyorejea upya.
Hatua hiyo imekuja huku Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, akiendelea kuwa rumande kwa zaidi ya mwaka sasa kutokana na kukabiliwa na tuhuma za uhaini.
No comments:
Post a Comment