Mfanyabiashara marufuu Kanda ya Ziwa, Christopher Mwita Gachuma (mwenye shati la drafti) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya programu ya AWE mkoani Mara, juzi.
------------------------------------------------Na Mwandishi Wetu, Mara
---------------------------------------
TAKRIBAN wanawake wajasiriamali 30 mkoani Mara wanashirki katika mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wa kibiashara, chini ya programu ya Chuo cha Wanawake Wajasiriamali (Academy for Women Entrepreneurs - AWE).
Mafunzo hayo ya miezi mitatu, yalianza wiki iliyopita katika Hoteli ya CMG iliyopo wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Programu hiyo ya AWE inafadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia ubalozi wake nchini Tanzania.
Mbali na kupata ujuzi wa kuendesha biashara, washirki mafunzo hayo pia watajengewa uwezo wa kuandika maandiko miradi ya kibiashara, kisha kupata fursa ya kutuma kuomba ruzuku katika Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania unaofadhili mafunzo hayo.
Washiriki wakifuatilia mada mafunzoni
Baada ya mafunzo hayo washiriki wataandika andiko la mradi kwa USDF ambako majina ya washindi yatatangazwa baada ya uhakiki kukamilika.
Pia washiriki wa mafunzo hayo wanaweza kutuma maandiko miradi yao kuomba ruzuku kwenye taasisi za kifedha na nyingine zinazoweza kuwasaidia kujiendeleza kiuchumi.
Wakufunzi wafafanua
“Mafunzo haya yatachukua miezi mitatu, kuanza Oktoba hadi Desemba mwaka huu. Washiriki walipata taarifa za mafunzo haya kupitia mtandao maalumu wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania,” alisema Kessia Kiwia, mmoja wa wakufunzi wa mfauzo hayo.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania anatajarajiwa kukutana na washiriki kabla ya kuhitimu mafunzo hayo, kwa mujibu wa Kiwia.
Ushuhuda wa wanufaika
Baadhi ya wanawake waliokwisha kunufaika na programu ya AWE kutoka mkoani Mwanza, wamefika kuonana na washiriki wa mafunzo hayo ili kutoa ushuhuda jinsi walivyonufaika nayo.
Esther Morris
“Faida za mafunzo haya ni nyingi sana, mfano mimi kabla sijayapata nilikuwa sijafanya biashara yangu kuwa halali, hivyo nilijifunza umuhimu wa kuhalalisha biashara, kupanga bei na namna ya kutangaza biashara yangu.
“Lakini kikubwa zaidi, nilipata ruzuku ya Dola 10,000 kutoka USADF (United States African Development Foundation) zikanisaidia kufungua ‘car wash’ yangu jijijini Mwanza na ninaendelea vizuri,” alisema Esther Morris, mmilki wa mradi wa Millagro Car Wash katika eneo la Misheni jijini la Mwanza.
Kwa upande wake Doreen Reuben ambaye pia ni mnufaika wa programu ya AWE alisema: “Haya mafunzo ni mazuri, yanamjengea mtu uwezo wa kufanya biashara na ujasiri pia.”
Doreen Reuben
Ushawishi wa Gachuma
Ushawishi wa kuelekeza mafunzo hayo mkoani Mara ulitolewa na mfanyabiashara maarufu Kanda ya Ziwa, Christopher Mwita Gachuma baada ya kuona faida zake kwa wanufaika wa programu hiyo waishio mkoani Mwanza.
“Nilihudhuria mafunzo kama haya jijijini Mwanza kama msemaji (speaker) na baada ya hapa nikawa impressed (nikafurahishwa) na kuona umuhimu wa wanawake wa mkoa wa Mara kuyapata, ndipo nikaamua kuwa sehemu ya wafadhili wake,” Gachuma alisema katika mahojiano na Gazeti la Sauti ya Mara mjini Tarime juzi, wakati alipopata fursa ya kuwatembelea washiriki wa mafunzo hayo.
Gachuma ambaye pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka Mkoa wa Mara, ndiye aliyefungua mafunzo hayo ya mkoani Mara na kuwataka washiriki hao kutumia fursa hiyo vizuri ili waweze kupata mwanga mzuri wa kuwa wajasiriamali wenye mafanikio.
“Uzuri ni kwamba kila mshiriki ana wazo tofauti, utakuta kuna watu wenye mawazo ya kukausha hata samaki,” alisema Gachuma ambaye pia amechangia ufadhili wa mafunzo hayo kwa kuwapa ukumbi wa kutumia katika hoteli yake ya CMG.
Matarajio ya washiriki
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kutapokea kwa mikono miwili, watarajia kupata mbinu bora zitakazowawezesha kufanya vizuri katika biashara zao.
“Ninatarajia baada ya kupata mafunzo haya nitaenda kufanya mapinduzi makubwa kwenye mradi wa kilimo biashara, matajiri wengi katika dunia na Tanzania hii miaka ijayo watatoka kwenye sekta ya kilimo,” alisema Pasikazia Msuke, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo.
Mshiriki mwingine Catherine Rugera, ambaye ni muuzaji wa dagaa aliowaita wazuri wa kukaanga wanaovuliwa katika Ziwa Victoria, alisema kwa tabasamu kubwa: “Kikubwa katika hii programu ya AWE nategemea kupanua biashara yangu na katika masoko ya ndani na nje ya Tanzania.
Naye Prisca William alisema anatarajia mafunzo hayo yatamjengea uwezo wa kujikita zaidi kwenye biashara za mtandaoni, akitumia fursa ya ukuaji wa teknolojia.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment