NEWS

Sunday 8 October 2023

Mkurugenzi wa HSF atoa angalizo kwa wazazi kuepusha watoto wao na vitendo vya ukatili



Mkurugenzi wa HSF, Emmyliana Range.
--------------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
--------------------------------------------


INA mandari nzuri, huduma bora, walimu wabobezi na miundombinu ya kisasa inayokidhi mahitaji ya kielimu kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne. Hii si nyingine yoyote, ni Shule ya Sekondari Maryo iliyopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara. 

Maryo ndiyo sekondari pekee ya bweni katika ukanda wa Nyamongo, na ambayo imejijengea sifa na uaminifu mkubwa kwa utoaji wa elimu bora ya darasani na ujasiriamali kwa wanafunzi. 

Alhamisi iliyopita, shule hii ambayo ni ya bweni na kutwa, ilisherehekea Mahafali ya Kwanza ya Wahitimu 20 (wavulana 13 na wasichana saba) wa Kidato cha Nne, huku ikijivunia mafanikio ya kitaaluma na huduma bora kwa wanafunzi wake. 

Wakisoma risala kwa mgeni rasmi katika mahafali yao yaliyofanyika shuleni, wahitimu hao walitaja mafanikio ya kitaaluma kuwa ni pamoja na kupata ufaulu wa daraja A (Division One) katika Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Pili kwa miaka miwili mfululizo (2021 na 2022). 

Aidha, walitaja huduma bora zitolewazo kwa wanafunzi shuleni hapo kuwa ni maji safi ya bomba, chakula bora, umeme, majengo ya kisasa yakiwemo mabweni, madarasa, maabara, bwalo la chakula na nyumba za walimu. 

Akizungumza katika mahafali hayo, Mkurugenzi wa Health and Safe Delivery Baby Foundation (HSF), Emmyliana Range alitoa wito wa kuhamasisha wazazi na walezi ndani na nje ya Nyamongo kupanga kupeleka watoto wao kusoma katika shule hiyo. 


Mkurugenzi Emmyliana (katikati), CEO wa Taasisi ya Maryo, Mariam Marwa Ryoba (kushoto) na Mkuu wa Sekondari Maryo, Laurian Thomas Kajanja wakiwasili kwenye sherehe za mahafali hayo shuleni hapo, Alhamisi iliyopita

Mkurugenzi Emmyliana alisema mbali na kuimarisha utoaji wa elimu na huduma bora, uongozi wa Shule ya Sekondari Maryo umeweka utaratibu mzuri wa kukusanya ada bila kusababisha bughudha kwa wazazi na wanafunzi.

“Hivyo wazazi na walezi mna kila sababu ya kuiamini sekondari hii ya Maryo na kuleta watoto wenu kupata elimu na huduma bora hapa bila kusita,” alisema. 

Alitumia nafasi hiyo pia kuwahimiza wazazi kuhakikisha wahitimu hao watakaporudi nyumbani wanapata malezi bora ili waendelee kuwa kioo cha jamii kwa nidhamu na maadili mema. 

"Wazazi lindeni watoto wenu, msiwapeleke kuishi kwa ndugu zenu, kaeni na watoto wenu nyumbani mkiwapatia malezi bora," alisisitiza Mkurugenzi Emmyliana. 

Pia aliwakumbusha wazazi na walezi kuwaombea wanafunzi hao baraka ya Mungu, hasa kipindi hiki wanachoelekea kufanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwezi ujao. 

Kwa upande mwingine, Emmyliana aliwatia moyo wahitimu hao, akisema walimu wa shule hiyo wamejipanga ipaswavyo kuwaimarisha kitaaluma ili waweze kupata ufaulu wa kishindo katika mtihani huo. 

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo wa Taasisi ya HSF aliwataka wanafunzi hao kuongeza bidii ya masomo na kudumisha nidhamu kwa walimu na wazazi. “Masomo na nidhamu ni vitu vinavyotegemeana,” alisema. 

Katika hatua nyingine, Emmyliana aliwasilisha mchango wa shilingi milioni tano taslimu uliotolewa na Mkurugenzi wa Lumry Company, Lucy Marwa Ryoba kuchangia ujenzi wa chumba cha masomo ya kompyuta shuleni hapo. 

Mkurugenzi Emmyliana ndiye aliyemwakilisha Mkurugenzi Lucy kama mgeni rasmi katika mahafali hayo yaliyofana kwa aina yake. 

Wadau wengine kutoka taasisi mbalimbali na wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Maryo waliunga juhudi hizo kwa michango ya fedha na vifaa vya ujenzi kupitia harambee ndogo iliyoongozwa na Mkurugenzi Emmyliana. 

Mahafali hayo yalihudhuriwa pia na wakuu wa shule za sekondari za serikali zikiwemo Nyamongo na Ingwe, kitendo ambacho Emmyliana alikipongeza akisema kinaonesha jinsi Sekondari ya Maryo ilivyo na uhusiano mzuri na shule jirani na jamii kwa ujumla. 

Taasisi ya Maryo pia inamiliki shule maarufu ya Maryo Pre and Primary English Medium katika eneo hilo la Nyamongo. 

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages