Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni akimkabidhi mwananchi kitambulisho cha Taifa mjini Musoma, Mara leo Alhamisi.
---------------------------------------------
Mara Online News
-----------------------------
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema Serikali kupitia wizara hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha ifikapo Desemba 2023, kila Mtanzania aliyesajiliwa anapata kitambulisho cha Taifa.
Ameyasema hayo wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya ugawaji wa vitambulisho vya Taifa, katika hafla iliyofanyika mjini Musoma, mkoani Mara, leo Alhamisi.
Kwa mujibu wa Waziri Masauni, uzinduzi huo ni suluhisho la ucheleweshaji vitambulisho vya Taifa, ambavyo amesema vina umuhimu mkubwa katika kuwezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za kijamii.
Amesema Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeongeza kasi ya kuvizalisha na kuvisambaza vikiwa na ubora unaostahili.
“Baada ya uzinduzi huu wa leo, ugawaji utaendelea kwenye vitongoji, vijiji na mitaa, hivyo nitumie nafasi hii kuwaomba viongozi kwenye maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa maafisa wa NIDA,” alisema Waziri Masauni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda amesema maafisa wa NIDA wanapaswa kugawa vitambulisho hivyo kwa wananchi bila kikwazo chochote.
Hivyo amesema mwananchi yoyote atakayekutana na kikwazo, ikiwemo kuombwa fedha ili apate kitambulisho anapaswa kutoa taarifa kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya, au ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Mhandisi Ismail Rumatila, hadi sasa wananchi zaidi ya milioni 24 wameshasajiliwa na wanatarajiwa kupata vitambulisho vyao.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment