NEWS

Thursday 19 October 2023

Right to Play, AICT waendelea kuhamasisha haki za mtoto wa kike Serengeti, TarimeAfisa Mradi kutoka AICT Mara, Rebeca Bugota (kulia) na Mwl Sophia Range wakikabidhi kombe kwa washindi wa mashindano ya soka kwa wanafunzi wa kike katika kijiji cha Mangucha wilayani Tarime jana.
--------------------------------------------

Na Waandishi Wetu,
Serengeti na Tarime
----------------------------
 

SHIRIKA la Right to Play kwa kushirikiana na AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe limeendelea kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike, huku likipinga vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni katika wilaya za Serengeti na Tarime mkoani Mara. 

Kampeni hiyo iliendeshwa kupitia matamasha na mabonanza ya michezo na burudani mbalimbali kwa wanafunzi wa shule za msingi juzi na jana chini ya mradi wa Save her Seat, ikiwa ni sehemu kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike. 


Akizungumza katika tamasha lililokutanisha wanafunzi wa shule za msingi Burunga na Tumaini wilayani Serengeti, Afisa Mafunzo kutoka Right to Play, Ramadhan Ismail alisema jamii inapaswa kuwapa watoto wa kikike haki sawa na wa kiume, ikiwemo elimu bora. 

Kwa upande wake mgeni rasmi na Afisa Elimu Kata ya Uwanja wa Ndege, Mwl Ramadhan Kassim aliwataka wazazi kuheshimu ndoto za mtoto wa kike za kielimu na kuepuka kumgeuza kuwa kitega uchumi chao kwa kumuoza ili kujipatia mahari. 

“Muda umefika kwa jamii kubadilika na kumwona mtoto wa kike kama lulu na kuachana na mila zinazokandamiza,” alisema Mwl Ramadhan. Katika wilaya ya Tarime, kampeni hiyo ilifanyika katika kijiji cha Mangucha katani Nyanungu, mgeni rasmi, Mwl Sophia Ghati Range aliisisitiza jamii kuepuka vitendo vya ubaguzi, ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto wa kike. 

“Wazazi tubadilike, tuwathamini watoto wa kike na kutowabagua katika kupata elimu. Wazazi wangu wangejali ng'ombe nisingesimama hapa kuwa mgeni rasmi, ndoto yangu ingepotea. Hivyo tusiwakekete watoto wa kike, tuwanoe akili zao,” alisema Mwl Sophia. 

Naye Afisa Elimu Kata ya Nyanungu, Mwl Petro Kimito aliwahimiza wazazi na jamii nzima kutambua kuwa watoto wa kike wanastahili haki sawa na watoto wa kiume - kuanzia kwenye elimu hadi kwenye mahitaji mengine ya kimwili na kiroho. Awali, Afisa Mradi kutoka AICT Mara, Rebeca, alisisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuwajali watoto wa kike kwa kuwapa nafasi ya kupata elimu bora sawa na watoto wa kiume. 

“Tulinde nafasi ya mtoto wa kike anapokuwa shuleni ili asome amalize na kutimiza ndoto zake. Kama tunataka kupata matokeo mazuri lazima tuwekeze kwao na matokeo tutayaona, hata shamba usipoweka mbolea huwezi kupata mavuno mazuri,” alisema Rebeca. 

Michezo husishwa katika mabonanza hayo yaliyoandaliwa na Shirika la Right to Play kwa kushirikiana na AICT ni pamoja na mpira wa miguu na pete kwa wavulana na wasichana, riadha, maigizo, ngonjera na mashairi. Washindi walipewa zawadi mbalimbali. Mradi wa ‘Save her Seat’ unaotekelezwa na Right to Play kwa kushirikiana na AICT Dayosisi ya Mara unalenga kulinda na kutetea nafasi ya mtoto wa kike dhidi ya vikwazo na changamoto mbalimbali zinazoweza kuwakwamisha kutimiza ndoto zao katika nyanja ya elimu ili kufika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages