NEWS

Thursday 26 October 2023

Serikali yatoa bilioni 14 kugharimia ujenzi wa stendi ya kisasa Mara, Chandi amshukuru Rais SamiaMwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa.

Na Mwandishi Wetu, Mara
------------------------------------


SERIKALI imetoa shilingi zaidi ya bilioni 14 kugharimia ujenzi wa stendi ya mabasi ya kisasa ya mkoa wa Mara, amesema Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo, Patrick Chandi Marwa. 


“Tumepata pesa zaidi ya shilingi bilioni 14 kujenga stendi mpya ya kisasa Butiama katika eneo la Makutano [Ziro-Ziro],” Chandi alisema katika mazunguzmo na gazeti hili kwa njia ya simu. 

Alisema sanamu kubwa ya Baba wa Taifa na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwl Julius Kambarage Nyerere itajengwa kwenye eneo la stendi hiyo ambayo itakuwa ikitoa huduma kwa mamia ya wasafiri wa ndani na mataifa jirani kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). 

Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ujili ya kutekeleza mradi huo wa stendi. 

“Wana-Mara tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt Samia kwa kutupatia fedha kwa ajili ya stendi mpya ya kisasa, na hii itakuwa pia ni kumuenzi vizuri Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere,”alisema Chandi. 

Chandi pia alishukuru Serikali kwa kutoa shilingi zaidi ya bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) katika wilaya ya Bitiama. 

“Tunamshukuru sana pia Rais Samia kwa ajili ya miradi, ikiwemo Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere, sasa mkoa wetu unaenda kufunguka kiuchumi na maendeleo yataenda kwa kasi,” alisema Chandi ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa wanasiasa watulivu na wapenda maendeleo katika mkoa huo alikozaliwa Baba wa Taifa. 

Alisema utekelezaji wa mradi wa stendi mpya ya mabasi utaanza wakati wowote kuanzia sasa mara baada ya taratibu zote kukamilika. 

Stendi hiyo itajengwa eneo la Makutano maarufu kama Ziro Ziro, kilomita chache kutoka Daraja la Kirumi - Barabara ya Mwanza - Musoma - Tarime. 

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA 
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages