NEWS

Monday 9 October 2023

Waziri Bashungwa akagua ujenzi wa barabara ya lami Mogabiri-Nyamongo wilayani Tarime, ahutubia mkutano wa hadhara NyamwagaWaziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akihutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Nyamwaga, wilaya ya Tarime mkoani Mara, wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa barabara ya lami Mogabiri-Nyamongo leo Jumatatu.
---------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime –
Mara Online News
-------------------------------


WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya lami Mogabiri-Nyamongo yenye urefu wa kilomita 25 katika wilaya ya Tarime, mkoani Mara. 

Aidha, katika ziara yake hiyo ya leo Jumatatu, Waziri Bashungwa amehutubia mkutano wa hadhara wa wananchi uliofanyika Nyamwaga yalipo makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. 

Ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo na kumhakikishia mkandarasi anayeijenga kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha inamlipa kwa wakati ili aweze kuharakisha utekelezaji wa mradi huo. 


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles (aliyesimama) akizungumza katika mkutano huo.

Awali, akisoma taarifa ya mradi huo kwa Waziri Bashungwa, Mkurugenzi wa Miradi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Makao Makuu, Mhandisi Boniface Mkumbo amesema ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 30 na kwamba unatarajiwa kukamilika Januari 2024. 

Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya kizalendo ya Nyanza Road Works, kwa gharama ya shilingi bilioni 34.662 za mapato ya ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan. 

Viongozi wengine waliofuatana na Waziri Bashungwa katika ziara hiyo ni Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Chomete, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Solomon Shati, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM wa Wilaya ya Tarime, Marema Sollo na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya, Samwel Mangalaya, miongoni mwa wengine. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages