NEWS

Wednesday 11 October 2023

Viongozi wa kijamii walivyojipanga kusaidia kukomesha uvamizi mgodi wa Barrick North Mara



Malori yakiwa kazini katika mgodi wa Barrick North Mara

Na Mwandishi Wetu, Tarime
---------------------------------------


WAZEE wa mila, madiwani na wenyeviti wa serikali za vijiji wamesema wamejipanga kuanza kufanyia kazi ombi la Rais wa Barrick la kuunganisha juhudi katika kukomesha tatizo la kuvamia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime. 

Katibu wa wazee wa mila wa koo 12 zinazounda kabila la Wakurya wilayani Tarime, Mwita Nyasibora amedokeza kuwa wameitikia ombi hilo na kwamba kwa sasa wanajipanga kuweka mkakati mahususi wa kulifanyika kazi. 

“Tunataka tusaidie mgodi usivamiwe, sisi tunatoa rai kwamba watakaobainika pale watashughulikiwa na wazee wa mila wa koo 12,” alisema Nyasibora katika mazungumzo na mwandishi wa habari hizi wilayani Tarime juzi. 

Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum kutoka Kata ya Nyamwaga, Mariam Mkono alisema mgodi wa North Mara una mchango mkubwa wa kimaendeleo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, hivyo jamii nzima katika halmashauri hiyo inaguswa moja kwa moja na tatizo la uvamizi mgodini. 

“Sisi madiwani wa kata tano zilizo jirani na mgodi wa North Mara tutalibeba jambo hilo la uvamizi kulipeleka kwenye vikao vya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ili lizungumziwe na madiwani wote kwa sababu huo mgodi unailipa halmashauri yetu fedha za service levy (ushuru wa huduma), hivyo nayo pia ni sehemu ya huo mgodi. 

“Lakini pia kuna fedha za CSR (Uwajibikaji kwa Jamii) ambazo zinatolewa na huo mgodi kusaidia uboreshaji wa huduma za kijamii - kuanzia kwenye vijiji 11 vya kata tano zinazozunguka mgodi hadi kwenye kata 26 za Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. 

“Kwa hiyo hili jambo siyo la madiwani wa kata tano zilizo jirani na mgodi, ni jambo la Halmashauri ya Wilaya ya Tarime nzima, hivyo lazima tukubali kusaidia hili tatizo liishe ili kuulinda mgodi uendelee kutunufaisha, lakini pia na jamii yetu isiumie kutokana na uvamizi mgodini,” alisema Diwani Mariam. 

Aliongeza kuwa wanafikiria pia kufanya mikutano ya hadhara ya wananchi kwa ajili ya kuzungumza na vijana na wazazi, ikiwemo kuwaeleza madhara ya uvamizi mgodini. 

Diwani Mariam alidokeza kuwa suala la uvamizi mgodini pia litakuwa ajenda ya kudumu kwenye vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) iliyoanzishwa na Barrick kwa lengo la kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wenyeji kutokana na fedha za mpango wa CSR. 

“Tukikubali kulisimamia jambo hili kwa juhudi za pamoja litakwisha. Tutakaa hadi na makundi ya vijana pamoja na uongozi wa mgodi wa North Mara ili kupata ufumbuzi wa tatizo hili la uvamizi mgodini,” alisema. 

Kiongozi huyo alisisitiza kuwa tatizo hilo lazima likomeshwe ili pia kuepusha madhara kwa wavamizi wenyewe ambao wakati mwingine huumizana kutokana na kugombea mawe ya dhahabu mgodini. 

“Uvamizi mgodini una madhara makubwa hata kwa watu wetu wenyewe, utakuta baadhi yao wanakufa na wengine wanapata vilema, na hata mtu anaweza akadondoka wakati anaruka ukuta akadondoka. Kwa bahati mbaya sana hata wanawake siku hizi wanakwenda usiku huko, si vijana peke yake. 

“Kibaya zaidi unakuta mwenzao akipata jiwe watampiga na hata wanaweza wakamuua kama hana nguvu za kujihami, wanatumia pia ubabe. Wanaenda pamoja lakini wakifika kule wanageukana. Hivyo hata wao wenyewe wanakatana mapanga wanaumizana. 

“Kwa hiyo tunataka tukutane na vijana hao tuzungumze nao, tujue changamoto zao, tuwaeleze madhara ya kuvamia mgodi, tuzungumze pia na wamama katika vijiji vinavyozunguka mgodi ili tujue tunaweza kusaidianaje kwa ajili ya kulinda mgodi wa North Mara, kwa sababu ni sehemu yetu pia, unatufanyia mambo makubwa sana ya kimaendeleo,” alisema Diwani Mariam. 

Kwa upande mwingine, wenyeviti wa vijiji vilivyo jirani na mgodi huo wameweka mkakati wa kukemea uvamizi huo sambamba na kuwaeleza wananchi wa maeneo yao ya uongozi madhara ya uhalifu huo. 

“Tumeweka mkakati, tunataka tuanze ziara kwenye vijiji vyote vinavyozunguka mgodi kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya kufanya uvamizi mgodini,” alisema Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyangoto, Mwl Mwita Msegi. 

Mwl Msegi alisema watashirikisha viongozi vitongoji, watendaji wa vijiji na kata, madiwani, wazee wa kimila na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya katika utekelezaji wa mkakati huo. 

Hivi karibuni, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Barrick, Mark Bristow aliwaomba viongozi wa serikali, kisiasa na kijamii wilayani Tarime kushirikiana na mgodi wa North Mara katika juhudi za kukomesha uvamizi mgodini unaofanywa na makundi ya watu wanaojulikana kama ‘intruders’. 

“Kama ambavyo nimekuwa nikipokea maombi yenu mengi na kuyatekeleza, na mimi nina ombi moja kwenu; ombi langu ni kwa kila mmoja wetu, kwamba tufanye kazi kwa pamoja kutokomeza hii tabia (uvamizi mgodini),” Bristow alisema katika mkutano ambao pia ulihudhuriwa na viongozi hao, mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele. 

Baadaye katika hutuba yake, DC Mntenjele alimhakikishia kiongozi huyo wa Barrick kuwa juhudi kubwa zitafanyika kukomesha uvamizi huo. 

“Uvamizi mgodini ni jambo ambalo hatupendezwi nalo. Tutafanya mikutano ya kuelimisha vijana kuachana na vitendo hivi ili wajihusishe kwenye shughuli mbadala kama kilimo badala ya kutegemea uvamizi mgodini,” alifafanua. 

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni Twiga Minerals. 

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages