NEWS

Wednesday 15 November 2023

Chandi amtumia Rais Samia salamu na shukrani za wana-Mara kupitia kwa Makonda



Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa.
--------------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
Mara Online News
-------------------------


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, ameongoza wananchi wa mkoa huo kumpokea na kumkaribisha kiongozi wa kitaifa wa chama hicho tawala, Paul Makonda, na kumuomba amfikishie Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan salamu na shukrani za wana-Mara.

Makonda aliyepata kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, aliteuliwa na kuidhinishwa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuwa Katibu wa Halmashauri hiyo, Itikadi, Uenezi na Mafunzo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Makonda kwenye uwanja wa Serengeti “Shamba la Bibi” mjini Tarime jana Jumanne, Chandi alimhakikishia kiongozi huyo wa CCM ngazi ya Taifa kuwa wana-Mara wako imara na wanamuunga Rais Samia mkono katika juhudi za kuwaletea Watanzania maendeleo ya kiskta.

“Katibu Mwenezi Taifa, ninakukaribisha, mkoa wa Mara ni imara, na utufikishie salamu kwa Mama Samia, umwambie mkoa wa Mara tunamuunga mkono na tunamshukuru sana kwa miradi mingi ya maendeleo katika mkoa wetu na Tanzania kwa ujumla,” Chandi alimwambia Makonda.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho, aliwasilisha kwa Makonda ombi la kugawa mkoa wa Mara kuwa mikoa miwili, na kupendekeza mkoa mpya uitwe Tarime, ombi ambalo kiongozi huyo wa kitaifa alilipokea na kuahidi kulifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia.

Makonda (kushoto) akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo, miongoni mwa viongozi wengine wa CCM na Serikali mkoani Mara jana Jumanne.
-------------------------------------------------
Kupitia mkutano wake huo wa mjini Tarime, Makonda alimwagiza Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda, kuingilia kati ili pikipiki (bodaboda) zilizokamatwa na Jeshi la Polisi katika mji wa Sirari mpakani na nchi ya Kenya, ziachiwe na kukabidhiwa kwa wamiliki husika kufikia leo Jumatano.

"Kuanzia sasa Mhe. Mtanda ifikapo kesho [leo Jumatano] pikipiki zote zilizokamatwa Sirari warudishiwe wenye pikipiki zao, na kama kuna mali zilizokamatwa watozwe kodi wapewe mali zao, na kuanzia hapo utaratibu wa kisheria ufuate mkondo wake," alisema Makonda.

Sambamba na hilo, Katibu huyo wa NEC ya CCM Taifa alimwagiza RC Mtanda kushughulikia haraka utatuzi wa migogoro ya ardhi inayoelezwa kukithiri katika maeneo mbalimbali mkoani humo.

Makonda alihitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Mara jana Jumanne.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages