Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof Lesakiti Mellau.
WETU, MJNUAT
---------------------------
HATIMAYE Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kilichopo Butiama mkoani Mara, kimeanza kufanya udahili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2023/2024.
Udahili huo ulianza Oktoba 13, 2023 baada ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kukiruhusu chuo hicho kufungua dirisha la udahili ambalo linatarajiwa kufungwa Novemba 14, 2023.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof Lesakiti Mellau amethibitisha kuwa TCU imekifungulia chuo hicho dirisha la kudahili wanafunzi na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania.
“Tumeshafunguliwa dirisha la waombaji kwa wanafunzi watarajiwa, dirisha lilifunguliwa pamoja na vyuo vingine (dirisha la nne), na chuo kimeongezewa muda wa dirisha kuwa wazi hadi tarehe 14 Novemba, 2023 ili wanafunzi wengi waweze kuomba,” alisema Prof Mellau wakati wa warsha ya kushirikisha wadau katika Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) mkoani Tabora, juzi.
Alibainisha kuwa chuo hicho kinatarajia kudahili wanafunzi wasiozidi 150 katika programu tatu za Shahada ya Sayansi ya Kompyuta, Shahada ya Sayansi katika Kilimo Uchumi na Kilimo Biashara, na Shahada ya Sayansi katika Elimu ya Viumbe Hai vya Majini.
“Tumeamua kuchukua wanafunzi 150 kwa sababu kwanza idadi hiyo ni nzuri kwa mwalimu kufundisha kivitendo na pili ni kutokana na nafasi ya kulala wanafunzi kulingana na miundombinu iliyopo,” alifafanua.
Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kimeanza kufanya udahili wa wanafunzi kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015, baada Serikali kutoa shilingi billion 2.661 kwa ajili ya kukarabati Kampasi ya Oswald Mang’ombe mwishoni mwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment