NEWS

Sunday 5 November 2023

Kewanja FC yaendelea kuwika Barrick North Mara Mahusiano Cup



Wachezaji na viongozi wa Kewanja FC wakishangilia ushindi baada ya kuichapa Kerende FC bao 1-0 na kutwaa ubingwa wa mashindano ya Barrick North Mara Mahusiano Cup mjini Nyamongo, Tarime jana Jumamosi.
------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Nyamongo
--------------------------------------------------

TIMU ya Kewanja FC imeendelea kuwika katika mashindano ya soka ya Barrick North Mara Maghusiano Cup, baada ya kuichapa Kerende FC bao 1-0 na kutetea ubingwa wa mashindano hayo kwa mara ya tatu mfululizo.

Mechi ya fainali ya mashindano hayo ilichezwa jana Jumamosi kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe uliopo Nyamongo, kilomita chache kutoka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Mgeni rasmi katika fainali hiyo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Matenjele ambaye alikabidhi zawadi ya kombe na fedha taslimu kwa timu ya Kewanja FC, na pia zawadi ya fedha taslimu kwa mshindi wa pili (Kerende FC) na wa tatu (Mrito FC).


Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Michael Mntenjele (katikati) na Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi wakikabidhi kombe kwa Geofrey Emmanuel ambaye ni Kepteni wa Kewanja FC.

Wengine waliopata zawadi ya fedha taslimu ni mwamuzi bora, Jacob Odongo, kocha bora, mchezaji bora, kipa bora, timu iliyoonesha nidhamu na mtangazaji bora wa mashindano hayo, Frank Jackson Chacha.

Wakati huo huo, mashindano hayo ya mwaka huu yamewezesha upatikanaji wa wachezaji 37 watakaounda timu mpya itakayoitwa North Mara FC.

Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano hayo, Mwita Marwa Magige, alisema wachezaji hao ni ambao wameonesha ubora na vipaji mahiri katika mashindano hayo.

Wachezaji wa Kewanja FC na Kerende FC wakichuana uwanjani.

Mwita ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyamwaga alisema wachezaji hao wakiwemo magolikipa watatu wameteuliwa kutoka timu mbalimbali zilizoshiriki mashindano hayo.

Mechi ya fainali ya mashindano hayo ilifana na kuwa kivutio kikubwa kutokana na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi kutoka vijiji na kata zinazozunguka mgodi wa North Mara.


Sehemu ya mashabiki na wachezaji wa akiba wakifuatilia mtanange huo uwanjani.

Viongozi wengine waliohudhuria fainali hiyo ni Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Baarick North Mara, Francis Uhadi aliyemwakilisha Meneja Mkuu wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko, na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara ambaye alitoa ahadi ya kuipeleka Bungeni timu mpya ya North Mara FC.

Pia alikuwepo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ulipo mgodi wa North Mara, Solomon Shati na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo, miongoni mwa viongozi wengine wa Serikali na jamii.

Mashindano ya Barrick North Mara Mahusiano Cup 2023 yalizinduliwa kwenye uwanja huo huo Septemba 29, mwaka huu na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Barrick, Mark Bristow. Kaulimbiu ya mashindano hayo inasema: “Mahusiano Bora kwa Uwekezaji Endelevu”.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages