Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi (kushoto) akiongoza Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara na viongozi wengine kuingia uwanjani kukabdhi zawadi kwa washindi wa fainali ya Mahusiano Cup 2023.
-------------------------------------------------
Nyamongo
------------------------------
VIONGOZI wa Serikali na jamii wamesema mashindano ya soka ya Mahusiano Cup yana nafasi kubwa ya kuboresha mahusiano kati ya Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara na jamii inayouzunguka.
Wakizungumza na Sauti ya Mara kabla na baada ya mechi ya fainali ya Mahusiano Cup 2023 mjini Nyamongo, Tarime juzi Jumamosi, viongozi hao waliwapongeza waandaaji na wadhamini wa madhindano hayo, wakisema yatakuwa chachu ya kuinua uchumi na uwekezaji endelevu katika eneo hilo.
Mashindano hayo ambayo yalizinduliwa na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Barrick Septemba 29, mwaka huu, yaliandaliwa na kudhaminiwa na Mgodi wa Barrick North Mara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Kampuni ya Barrick inatumia mashindano hayo kukuza na kudumisha mahusiano mema kati ya mgodi wake wa North Mara na jamii inayouzunguka.
Lengo kuu ni kuona mashindano hayo yanasaidia kuongeza uelewa juu ya fursa mbalimbali zilizopo na kushughulikia masuala mtambuka, hasa uvamizi mgodini, uharibifu wa miundombinu (vandalism) na utegeshaji wa mazao, miti na nyumba kwenye maeneo yanahitajika kwa ajili ya upanduzi wa shughuli za mgodi huo.
Mwl Mwita Msegi ambaye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyangoto kilichopo jirani na mgodi wa North Mara, anasema uendelevu wa mashindano ya Mahusiano Cup utasaidia kupunguza vitendo vya kuvamia mgodi vinavyofanywa na makundi ya watu - maarufu kwa jila la ‘intruders’.
“Binafsi ninaupongeza sana mgodi wa Barrick North Mara kwa kuona umuhimu wa kuandaa na kudhamini mashindano ya Mahusiano Cup, na ninaamini kwamba hatua hii itasaidia kupunguza intruders mgodini,” alisema Mwl Msegi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyamwaga, Chacha Michael Babere, alisema mashindano ya Mahusiano Cup ni fursa kwa viongozi, vijana na makundi mengine kukutana, kufahamiana, kujenga mahusiano na kuelimishana masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Mahusiano Cup 2023, Mwita Marwa Magige, alisema yamekuwa chachu ya kuibua vipaji vya michezo miongoni mwa vijana wanaoishi katika vijiji vilivyo jirani na mgodi wa North Mara.
Mfano, alisema mashindano ya Mahusiano Cup 2023 yamewezesha upatikanaji wa wachezaji 37 watakaounda timu mpya itakayoitwa North Mara FC.
“Wachezaji ambao wameoteuliwa kuunda timu mpya ya North Mara FC ni ambao wameonesha ubora na vipaji mahiri katika mashindano hayo,” alisema Mwita ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyamwaga.
Alifafanua kuwa wachezaji hao wakiwemo magolikipa watatu wameteuliwa kutoka timu mbalimbali zilizoshiriki mashindano hayo.
Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara alisema mashindano hayo yatahamasisha ushirikiano kutoka kwa jamii inayozunguka mgodi wa North Mara ili kuwezesha pande zote mbili kunufaika na uwekezaji kwenye mgodi huo.
Waitara alitumia nafasi hiyo pia kutoa ahadi ya kuwapeleka Bungeni Dodoma wachezaji wa timu ya North Mara FC.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele ambaye alikuwa mgeni rasmi katika fainali ya Mahusiano Cup 2023, alitoa wito wa kuhamasisha vijana kujitokeza kwa wingi kuonesha vijapi vyao kupitia mashindano hayo.
“Michezo ni afya, michezo ni ajira na michezo inajenga mahusiano mema na amani katika jamii,” alisema DC Mtenjele.
Kaulimbiu ya Mashindano ya Barrick North Mara Mahusiano Cup 2023 inasema: “Mahusiano Bora kwa Uwekezaji Endelevu”.
Timu zilizoshirikia mashindano hayo ni kutoka vijiji vilivyo jirani na mgodi wa North Mara zikiwemo Genkuru, Msege, Komarera, Nyamwaga, Kewanja, Nyakunguru, Kerende, Nyabichune, Mjini Kati, Matongo, Nyangoto, Mrito, Keisangora na Nyarwana.
Katika mechi ya fainali hiyo iliyochezwa juzi Jumamosi kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe, timu ya Kewanja FC iliichapa Kerende FC bao 1-0 na kutetea ubingwa wa mashindano hayo kwa mara ya tatu mfululizo.
Wachezaji na mashabiki wa Timu ya Kewanja FC wakishangilia ushindi wa Mahusiano Cup 2023 kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe, juzi Jumamosi.
Mechi hiyo ilifana na kuwa kivutio kikubwa kutokana na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi kutoka vijiji na kata zinazozunguka mgodi wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara.
DC Matenjele alikabidhi zawadi ya kombe na fedha taslimu kwa timu ya Kewanja FC, na zawadi ya fedha taslimu kwa mshindi wa pili (Kerende FC) na wa tatu (Mrito FC).
Wengine waliopata zawadi ya fedha taslimu ni mwamuzi bora, Jacob Odongo, kocha bora, mchezaji bora, kipa bora, timu iliyoonesha nidhamu na mtangazaji bora wa mashindano hayo, Frank Jackson Chacha.
Matumaini ya viongozi na wananchi wa wilaya ya Tarime ni kwamba Barrick North Mara pia watafikiria umuhimu wa kupanua wigo wa michezo kwa kuanzisha mashindano ya michezo mingine kama mpira wa mikono, kikapu, kukimbia na kadhalika.
Viongozi wengine waliohudhuria fainali hiyo ni Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Baarick North Mara, Francis Uhadi aliyemwakilisha Meneja Mkuu wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko.
Pia walikuwepo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ulipo mgodi wa North Mara, Solomon Shati na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo, miongoni mwa viongozi wengine wa Serikali na jamii.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment