Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa akizungumza katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Butiama wakati wa ziara yake hivi karibuni.
--------------------------------------------------------
MAALUM, Mara
---------------------------
Ni ziara ya kishindo cha aina yake. Ndivyo tunavyoweza kuelezea ziara ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara ya kuimarisha chama mkoani hapa.
Chandi pia amepata fursa ya kukagua miradi ya chama hicho tawala na kusikiliza kero za wananchi katika majimbo ya Musoma Mjini, Musoma Vijijini, Butiama, Serengeti, Tarime Vijijini na Tarime Mjini.
Katika ziara hiyo iliyohitimishwa wiki iliyopita, Chandi aliambatana na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mara, wakiwemo wabunge, wenyeviti na makatibu wa wilaya.
Akiwa Butiama alikoanzia ziara hiyo, Mwenyekiti huyo Pamoja na mambo mengine, alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi ya CCM Tawi la Kitaramanka na kutoa msaada wa saruji kuchangia ujenzi huo.
Aidha, baada ya kusikiliza kero za wananchi aliwaagiza viongozi wa wilaya ya Butiama kuzitafutia ufumbuzi, huku akitumia nafasi hiyo pia kupiga marufuku makundi ndani ya CCM.
Wananchi wa wilayani Butiama wakimsikiliza Mwenyekiti Chandi (hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara.
Siku iliyofuata, Chandi alikwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi ya CCM Wilaya ya Musoma Vijijini kabla ya kushiriki kikao cha ndani cha chama hicho.
Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuwapuuza viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani wanaowachochea kutochangia shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
“Nchi hii hapa tulipo ni pazuri, wapuzeni hao wanaotwambia mambo ya Ulaya. Unaambiwa usichangie shughuli za maendeleo, wanataka mkwame. Mkishikamana maendeleo yataenda kwa haraka,” alisema Waitara.
Alisema kata nyingi mkoani Mara zimepata maendeleo kwa sababu madiwani na wabunge wanatokana na CCM.
“Wapinzani ninawajua nje na ndani, wanachofanya wanachemsha mawe, ni ndege wasiofugika, kunguru asiyepikwa, akipikwa haivi, akiiva hanyweki supu wala kuliwa. Adui yako hawezi kukuchagulia rafiki, hata kwenye bandari tungewasikiliza tungekwama,” alisema.
Katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Chandi, alitoa maelekezo ya kushughulikia utatuzi wa kero mbalimbali za wananchi katika jimbo la Musoma Vijijini.
Akiwa katika jimbo la Serengeti, kiongozi huyo wa mkoa alikagua na kushiriki kwa vitendo ujenzi wa jengo la nyumba ya makazi ya Katibu wa CCM Wilaya.
Baadaye Chandi alikwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi ya CCM Tawi la MCU, kabla ya kutembelea jengo la kitega uchumi cha chama hicho lililopo mjini Mugumu.
Katika hatua nyingine, Chandi alitoa maelekezo ya kushughulikia utaratibu wa kuligawa jimbo la Serengeti kuwa majimbo mawili ya uchaguzi.
Alimwagiza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma kushughulikia suala hilo kupitia vikao vya madiwani.
“Ninakuagiza uitishe kikao cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kugawa jimbo hili tupate wabunge wawili katika uchaguzi ujao,” alimwagiza Makuruma wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Serengeti kilichofanyika mjini Mugumu.
Kwa mujibu wa Chandi, jimbo la Serengeti likigawanywa Serikali italiongezea bajeti ya kuboresha barabara ambazo hazifanyiwi ukarabati kutokana na ufinyu wa bajeti.
Hivi karibuni, Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti walitoa azimio la kuitaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) kuipatia halmashauri hiyo fedha za dharura kwa ajili ya matengenezo ya barabara zisizopitika kwa sasa.
Kikao hicho cha madiwani kiliazimia kwamba TARURA ifanye maombi maalum ya fedha ambazo zitasaidia kugharimia matengenezo ya barabara ambazo hazipitiki katika wilaya hiyo ambayo sehemu yake kubwa imepakana na maeneo ya hifadhi za wanyamapori, ikiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti.
“Barabara zetu nyingi hazipitiki na ndio maana madiwani leo wamekuwa wakali sana. Kwa kuwa tunaona bajeti ni ndogo kwa halmashauri yetu ya Serengeti ukilinganisha na halmashauri zingine za mkoa wa Mara,” alisema Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ayub Mwita Makuruma.
“Mtandao wetu wa barabara ni zaidi ya kilomita 971, na kati hizo, kilomita 386 kwa sasa hazipitiki kabisa,” alisema Makuruma ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Busawe kupitia chama tawala - CCM.
Aliongeza: “Ombi letu, bajeti iongezwe na tumetoa ushauri wa jumla kwamba maombi maalum yaandikwe na kutumwa mara moja kwa TARURA ili kunusuru hali ilivyo kwa sasa kwani ni mbaya sana.”
Mkazi wa mji wa Mugumu, Joel Magesa akiwasilisha kero kwa Mwenyekiti Chandi (hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara.
Kwa upande mwingine, Chandi alidokeza kuwa mipango ya kuanza ujenzi wa uwanja wa Ndege Mugumu iko katika hatua za mwisho kukamilika.
“Uwanja wa ndege utaanza kujengwa rasmi, mapato yataimarika, Mama [akimaanisha Rais Samia Suluhu Hassan] katoa fedha,” alisema.
Kwa mujibu wa Chandi, asilimia 80 ya eneo la Hifadhi ya Taifa Serengeti lipo ndani ya wilaya ya Serengeti, hivyo wakazi wake wanastahili kunufaika ipasavyo na mapato ya hifadhi hiyo.
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Serengeti ulitumia nafasi hiyo kumtunuku Mwenyekiti huyo tuzo maalum ya kutambua na kuthamini mchango wake mkubwa katika kukijenga na kukiimarisha chama hicho tawala wilayani humo na katika mkoa wa Mara kwa ujumla.
Chandi alikabidhiwa tuzo hiyo na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Serengeti, Morobanda Japan - ikitokea kwa Katibu wa UWT CCM Wilaya ya Serengeti, Mary Kananda (kulia).
Vile vile, Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Musoma Mjini kilimtunuku Chandi cheti cha pongezi kwa kuchaguliwa kwa kishindo, pamoja na kazi nzuri anazoendelea kufanya kuimarisha chama hicho na jumuiya zake mkoani Mara.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini, Benedictor Maregesi alimkabidhi Chandi cheti hicho katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho wilayani humo.
Chandi pia alipata fursa ya kusikiliza kero za wanachama na wananchi mbalimbali zikiwemo za uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, migogoro ya ardhi, kikokotoo kisicho rafiki kwa watumishi, kadi za bima ya afya kutothamiwa, mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano kutotibiwa bure kama Ilani ya CCM inavyoelekeza, kisha akatatua baadhi na nyingine kuzitolea maelekezo ya kuzitafutia uvumbuzi.
Alitumia nafasi hiyo pia kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuelekeza fedha nyingi mkoani Mara kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo Hospitali ya Rufaa Kwangwa.
Chandi aliwaomba wananchi kukipatia CCM ushindi mnono katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwakani, akisema ndicho chama kilichopewa dhamana kubwa ya kuhakikisha maendeleo ya kisekta yanapatikana nchi nzima.
“Mwakani tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, naomba tukipe CCM ridhaa kwa kura nyingi kiendelee kushika dola na kuongoza Serikali kwa maendeleo ya Watanzania kwa ujumla,” alisema Chandi.
Ziara yake katika wilaya ya Tarime ilikuwa na kionjo cha aina yake, baada ya makada kadhaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kujitokeza mbele yake na kutangaza kuachana na chama hicho cha upinzani, na kujiunga na chama tawa - CCM.
Mwenyekiti Chandi aliwapokea makada hao na kuwakabidhiwa kadi za uanachama wa chama tawala katika ofisi za CCM Wilaya ya Tarime.
Makada walioitosa CHADEMA na kujiunga na CCM wakionesha kadi mpya za uanachama.
Makada hao walitaja kilichowasukuma kuchomoka CHADEMA kuwa ni maendeleo makubwa ya kisekta yanayoletwa nchini na Serikali ya CCM, chini ya Rais Samia.
“Miradi ya kimkakati inayotekelezwa imenisukuma kufanya maamuzi ya kuwakimbia CHADEMA maana hawana dola, na wanagombana wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama. Niko tayari kukitumikia Chama Cha Mapinduzi,” alisema Richard Choso, mkazi wa mtaa wa Nyamisangura B mjini Tarime.
Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Much Know Mashauri na mkazi wa Nyamisangura pia alisema “Kazi kubwa zinaonekana - mwenye macho haambiwi tazama, nimepima nikatazama nikajivua gwanda.”
Baadaye Chandi aliwahimiza viongozi na wanachama wa CCM mkoani Mara kusimamia kwa vitendo utekelezaji wa Ilani ya chama hicho tawala.
Pia aliwataka kumaliza makundi ndani ya chama hicho, kutokwepa vikao ngazi ya matawi na kata, kuhamasisha na kusajili wanachama wapya.
Mwenyekiti Chandi akizungumza katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Tarime.
“Mama [Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan] ametuagiza tusimamie makundi yasiwe kwenye chama. Kama kuna changamoto zijadiliwe kwenye vikao halali, vikao vikikaa hakuna jambo gumu, hakuma mkate mgumu mbele ya chai,” alisema Chandi na kuendelea:
“Moja ya misingi ya CCM ni vikao, chama kisicho na vikao kinakua kimevunjika mikono na miguu, tukiimarisha vikao kwenye mashina na matawi tumeimarisha chama. Tunahamasisha chama na jumuiya zake za Vijana [UVICCM], Wazazi na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), ingizeni wanachama wapya.”
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment