NEWS

Sunday 26 November 2023

Kupungua kwa samaki Ziwa Victoria kwatajwa kuua viwanda vya minofu, wadau watahadharisha…



Minofu ya samaki aina ya sangara

Na Christopher Gamaina, Mara
--------------------------------------------


KUPUNGUA kwa samaki katika Ziwa Victoria kumetajwa kuwa ndiyo sababu kuu ya kufungwa kwa viwanda vya kuchakata minofu ya samaki mkoani Mara.

“Viwanda vimefungwa kwa sababu samaki hasa aina ya sangara sasa hivi hawapatikani kwa wingi ziwani kutokana na kuvuliwa hadi vifaranga kila siku, hawaachwi wazaliane na kukua,” mwekezaji mzawa wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba pembeni mwa Ziwa Victoria wilayani Rorya, Peter Mwera, aliiambia Sauti ya Mara mkoani hapa juzi.


Samaki wadogo aina ya sangara

Makamu wa Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) anayeshughulikia masuala ya biashara, Boniface Ndengo, alithibitisha kufungwa kwa viwanda vikubwa vya kuchakata minofu ya Samaki mkoani Mara.

“Mkoa wa Mara tulikuwa na viwanda vinne vikubwa, vitatu vimekufa - kimebaki kimoja kinachosuasua, hii ni kwa sababu samaki ambao ndio malighafi za viwanda hivyo wamepungua ziwani,” alisema Ndengo ambaye pia ni Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mara.

Alitaja madhara ya kufungwa kwa viwanda hivyo kuwa ni kuporomoka kwa uchumi wa mkoa huo, ukosefu wa ajira kwa vijana na kusababisha maisha magumu kwa wananchi.

Ndengo na Mwera wanatahadharisha kuwa hali ya upatikanaji wa samaki katika Ziwa Victoria itaendelea kuwa mbaya zaidi ikiwa mamlaka za Serikali hazitachukua hatua za haraka kudhibiti kasi ya uvuvi ukiwemo usio halali.

“Serikali ije na mikakati ya kuongeza ulinzi na teknolojia ya uvuvi ili kuongeza wingi wa samaki ziwani,” alisema ndengo.

Kwa upande wake, Mwera ambaye pia ni mwekezaji wa kiwanda kidogo cha kusindika samaki, alishauri Serikali irejeshe utaratibu wa kupumzisha shughuli za uvuvi ziwani kwa muda fulani ili kutoa nafasi kwa samaki kuzaliana na kukua.

“Serikali irudishe utaratibu wa likizo ya uvuvi hata ya miezi mitatu kwa mwaka ili kuongeza upatikanaji wa samaki, vinginevyo samaki wataisha kabisa katika Ziwa Victoria,” alisisitiza Mwera.

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages