NEWS

Tuesday 14 November 2023

Mbunge Chege awakilisha wana-Rorya kumpatia Makonda zawadi ya ng’ombe
Na Mwandishi Wetu
Mara Online News
----------------------------


MBUNGE wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege, ametoa zawadi ya ng’ombe (pichani juu) kumpatia Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda aliyekuwa katika ziara ya kikazi mkoani Mara.

Mbunge Chege amempatia Makonda ng’ombe huyo kama zawadi ya pongezi, kutambua na kukubali kazi kubwa aliyoanza kufanya tangu ateuliwe na kuidhinishwa na NEC ya CCM Taifa kushika nafasi hiyo ya uongozi ndani ya chama hicho tawala.

“Kwa niaba ya wananchi wa jimbo la Rorya ninampongeza Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kupendekeza na kumteua Ndg. Paul Makonda kushika nafasi hiyo,” alisema Mbunge Chege jana Jumanne, siku ambayo Makonda alihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Mara.

Mbunge huyo kijana alisema yeye na wana-Rorya wana imani na Makonda, na wanamuombea mafanikio tele katika majukumu mapya ya kukitumikia chama hicho tawala, kwa maendeleo ya Watanzania kwa ujumla.

“Tuna imani kubwa na Ndg. Makonda kama kijana mwenzetu kwa kazi nzito aliyopewa ya kukisemea na kukiimarisha chama, na tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema na atende yale yaliyo matarajio na matamanio ya Watanzania walio wengi, na kiukweli ameanza vyema,” alisema Mbunge Chege.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledia

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages