NEWS

Wednesday 29 November 2023

Peter Zakaria achangisha milioni 7.5 kuipiga jeki SACCOS ya KUBATA, adokeza siri ya mafanikio



Mfanyabiashara Peter Zakaria akizungumza wakati wa harambee ya kuchangia SACCOS ya KUBATA mjini Tarime jana Jumanne.
-------------------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News
-----------------------------

MFANYABIASHARA maarufu wa wilayani Tarime, Peter Zakaria ameongoza harambee ya kuipiga jeki SACCOS ya KUBATA na kufanikisha upatikanaji wa shilingi milioni 7.5.

Harambee hiyo ilifanyika jana Jumanne katika Hoteli ya Goldland mjini Tarime, Mara ambapo Zakaria pekee alichangia shilingi milioni tano na kuungwa mkono na rafiki zake kwa shilingi zaidi ya milioni moja.

Iliandaliwa na Taasisi ya Kuza Uchumi Boresha Afya Tanzania (KUBATA) kwa lengo la kupata shilingi milioni 15 kwa ajili ya kununua mashine ya mradi wa kusaga na kukoboa nafaka.


Sehemu ya wadau walioshiriki harambee hiyo

Katika hotuba yake, Zakaria ambaye alikuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo, aliwakumbusha viongozi husika kuzingatia uwazi, uaminifu na ushirikishaji wanachama katika suala zima la mapato na matumizi ya SACCOS hiyo.

“Vyama vingi vinaanzishwa vizuri, lakini baadaye ni matatizo, KUBATA SACCOS isifikie huko, ishirikishe wanachama muwe wamoja. Mtakapoanzisha miradi ya kusaga na kukoboa nafaka muwe mnatoa taarifa ya mapato na matumizi ili wanachama wawaelewe, mkifanya kinyume hamtaendeleza SACCOS,” alisema Zakaria.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa KUBATA, Chacha Getamuru alimshukuru Zakaria na wachangiaji wengine, na kutumia nafasi hiyo kutoa wito wa kuwakaribisha wakazi wa Tarime na maeneo mengine mkoani Mara kujitokeza kujiunga na SACCOS hiyo.


Mwenyekiti wa KUBATA Ltd, Chacha Getamuru akieleza la harambee hiyo.

Getamuru alitumia nafasi hiyo pia kuiiomba Serikali na wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuwashika mkono hata kwa kununua bidhaa zinazozalishwa na SACCOS ya KUBATA.

“Tunawakaribisha wananchi wa mkoani Mara kujiunga katika hii SACCOS, na tunaomba Serikali itushike mkono ili tutengeneze ajira na kuchangia pato la taifa. Pia wananchi na wadau watuunge mkono kwa kununua bidhaa zetu,” alisema.

Kwa mujibu wa Getamuru, hadi sasa SACCOS hiyo yenye makao makuu wilayani Tarime, ina wanachama zaidi ya 80 - ikijishughulisha na kuweka na kukopesha fedha, na kwamba tayari imewekeza shilingi milioni mbili kwenye mradi wa kusaga na kukoboa nafaka.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages