NEWS

Sunday 19 November 2023

RC Mara ataka ukaguzi mradi wa ujenzi Kituo cha Polisi Butiama



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda (katikati) akisisitiza jambo wakati alipokwenda kujionea ujenzi wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Butiama jana. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Moses Kaegele na kulia ni Mbunge wa Butiama, Jumanne Sagini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
--------------------------------------------------

NA MWANDISHI
WETU, Butiama
----------------------------


SERIKALI mkoani Mara imesema itakagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Butiama kilichotengewa shilingi milioni 802.

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda alitangaza msimamo huo alipokwenda kujionea hali halisi ya mradi huo, jana.

“Kupitia mkaguzi wetu wa ndani tutakagua takwimu na kiasi cha fedha kilichotumika, yaani mililioni 366 kama kinalingana na thamani ya fedha,” alisema RC Mtanda na kuongeza:

“Tutaishauri Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani mradi huu unaweza kuisha chini ya thamani hiyo iliyotajwa [milioni 802].”

Alifafanua kuwa shilingi milionni 366 zilizokwishatumika ni sehemu ya shilingi milioni 500 ambazo tayari zimetumwa na Serikali Kuu kupitia Akaunti ya Mkuu wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Mara.

Muonekano wa jengo la Kituo cha Polisi Wilaya ya Butiama linaloendelea kujengwa.
RC Mtanda alisema alilazimika kwenda kupata taarifa za ujenzi wa kituo hicho baada ya kuona kwenye mitandao ya kijamii kwamba fedha za mradi huo ‘zimepigwa’.

Katika ziara hiyo, kiongozi huyo wa mkoa alifuatana na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele na Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages