NEWS

Monday, 2 February 2026

Kemanyanki Day 2025: DC Gowele aipongeza kwa kubadili maisha ya vijana vijiji jirani na Mgodi wa North Mara



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akizungumza katika sherehe za Siku ya Kemanyanki, mjini Nyamongo, Januari 31, 2026. Aliyekaa kulia ni Mkurugenzi wa Kemanyanki, Nicolaus Mahando Mgaya - maarufu kwa jina la Chichache.

Na Christopher Gamaina
Tarime
--------------

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, ameipongeza Kampuni ya Kemanyanki Contractors Manpower and Supply Company Ltd, kwa mchango wake mkubwa katika kubadili maisha ya vijana na wakazi wa vijiji vinavyozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, kupitia ajira, elimu ya ujasiriamali na ustawi wa kijamii.

Amesema jitihada za Kemanyanki katika kuajiri mamia ya wananchi, wengi wakiwa vijana kutoka maeneo hayo, zimekuwa suluhisho la matatizo ya ukosefu wa ajira na uhalifu, ukiwemo wa kuvamia mgodi huo.

Aidha, ameipongeza kampuni hiyo kwa utaratibu wake wa kuwalipia wafanyakazi wake bima ya afya, na kuzitaka kampuni nyingine kuiga mfano huo ili kuunga mkono jitihada za serikali katika kulinda ustawi wa wafanyakazi.

DC Gowele alitoa pongezi hizo wakati akizungumza katika sherehe ya Maadhimisho ya Saba ya Siku ya Kemanyanki, yaliyofanyika Chichake Sports Bar & Grill, Nyamongo, Januari 31, 2026, ambapo alikuwa mgeni rasmi.

“Niwapongeze sana Kemanyanki kwa kuanzisha Kemanyanki Day. Hii ni siku muhimu inayojenga mshikamano, upendo na umoja miongoni mwa wafanyakazi, lakini pia inaleta uadilifu na kuimarisha imani, kwa sababu wafanyakazi wanajisikia kuwa wao ni sehemu ya kampuni.

“Niendelee kushauri kampuni nyingine kuwakutanisha watumishi kama hivi - wanafurahi na kusherehekea pamoja mafanikio yaliyopatikana, lakini pia inatoa nafasi ya kufanya tathmini ya wapi tulikuwa na mapungufu, na tufanye nini kuongeza ufanisi wa kazi zetu,” alisema DC Gowele.

Vilevile, aliwapongeza Wakurugenzi wa Kemanyanki kwa ubunifu wa mipango yao ya kimkakati, ikiwemo utoaji wa elimu ya ujasiriamali na ajira kwa vijana, wakiwemo waliokuwa wakijihusisha na vitendo vya uvamizi na uporaji wa mawe yenye dhahabu katika mgodi wa North Mara.

“Serikali tutaendelea kuunga mkono jitihada ambazo mnazifanya ili kuhakikisha mnapata fursa nyingi ambazo mnaweza kutoa ajira kwa watu wengi, kwa sababu naamini mkiendelea kupata fursa nyingi mtaendelea kutoa ajira nyingi kwa watu ambao wako mitaani.

“Mnachokifanya mnatupunguzia changamoto kubwa mitaani, kama hawa watu wote zaidi ya 140 wasingekuwa kwenye ajira rasmi pengine wangekuwa wahalifu,” DC Gowele aliwambia Wakurugenzi wa Kemanyanki.

Awali, Mkurugenzi wa Kemanyanki, Nicolaus Mahando Mgaya - maarufu kwa jina la Chichake, alisema kampuni hiyo inajivunia kuona vijana wengi, wakiwemo waliokuwa wakijihusisha na uvamizi wa mgodi wakibadilika na kuwa wafanyakazi waaminifu na wajasiriamali wenye mafanikio.

Kwa mujibu wa Chichake, kwa sasa baadhi ya vijana hao wamejenga nyumba za kudumu, wamenunua viwanja na kuanzisha biashara mbalimbali. “Wengi wa vijana tuliowaajiri wanapoacha kazi wanaanzisha biashara au kampuni zao binafsi na wanakuwa na mafanikio,” alisema.


Mkurugenzi Chichake akizungumza katika sherehe hizo

Kemanyanki ni kampuni ya wazawa inayofanya kazi na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Twiga Minerals.

Tangu kuanzishwa kwake, Kemanyanki imejijengea heshima kwa kutoa kipaumbele kwa ajira za wazawa, hatua iliyosaidia kupunguza ukosefu wa ajira, kukuza ujuzi na kuinua maisha ya familia nyingi katika jamii zinazozunguka mgodi huo.

“Tunaishukuru sana Kampuni ya Barrick kwa kutengeneza fursa endelevu za kunufaisha jamii inayozunguka mgodi wa North Mara,” alisema Chichache.

Ushirikiano unaotolewa na mgodi huo unatajwa kuwa chachu ya mafanikio ya kampuni hiyo na maendeleo ya jamii, ukidhihirisha namna sekta binafsi na wadau wa maendeleo wanavyoweza kushirikiana kwa manufaa ya wote.

“Mwaka 2025 tulifanya kazi bila kupata ajali yoyote ile - wafanyakazi wetu wote walitoka kwenda kazini na kurudi nyumbani salama,” alisema na kuweka wazi kuwa wafanyakazi 624 wamenufaika na ajira ndani ya Kemanyanki Contractors kati ya mwaka 2023 na 2025.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, asilimia 90 ya ajira zilizotolewa na Kemanyanki ziligusa wakazi wa vijiji vilivyo jirani na mgodi, huku asilimia 80 ya wafanyakazi hao wakiwa vijana.

“Asilimia 70 ya wafanyakazi wetu waliokuwa na hali duni - sasa hivi wamejenga makazi ya kudumu, na tunawapa motisha ya kuwakopesha vifaa vya ujenzi bila riba,” alisema Mkurugenzi Chichake.

Mbali na ajira, Kemanyanki imekuwa ikisaidia jamii kwa kuchangia vifaa vya shule, ikiwemo vya michezo, kusaidia ada na michango ya shule kwa baadhi ya wafanyakazi wake, pamoja na kufadhili walimu wa masomo ya sayansi katika shule zenye upungufu wa walimu hao.

“Tumekuwa tukitoa ufadhili wa kuwalipa walimu wa masomo ya sayansi katika shule zenye upungufu wa walimu hao,” alisema Chichake.

Hatua hizo zinaendelea kuifanya Kampuni ya Kemanyanki kuwa mfano wa kuigwa katika utoaji ajira na uwajibikaji kwa kijamii, hususan kwenye vijiji vinavyozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na wilaya ya Tarime kwa ujumla.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages