Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda (wa pili kulia) akioneshwa pikipiki zinazoshikiliwa katika kituo cha Polisi Tarime leo Jumatano. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele.
-------------------------------------------------
Mara Online News
----------------------------
MKUU wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda, ameanza kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda.
Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Tarime jana Jumanne, Makonda alimwagiza RC Mtanda kuhakikisha pikipiki zilizokamatwa na Jeshi la Polisi katika mji wa Sirari, mpakani na nchi ya Kenya zinaachiwa na kukabidhiwa kwa wamiliki husika baada ya kutimiza masharti ya kisheria.
Pia Makonda alimwagiza RC Mtanda kushughulikia utatuzi wa migogoro ya ardhi inayoelezwa kukithiri katika mkoa wa Mara.
Katika kuonesha uwajibikaji, leo Jumatano RC Mtanda amefuatana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele kwenda katika vituo vya Polisi Tarime na Sirari kuhimiza utekelezaji wa agizo la kuachia pikipiki zilizokamatwa.
“Waiteni wenye pikipiki hizi zenye makosa yasiyo ya jinai walipie faini muwakabidhi, wale wenye bidhaa za kula na simenti walipie ushuru wa Serikali muwape,” alisisitiza kiongozi huyo wa mkoa.
RC Mtanda (kushoto) akikagua saruji zilizokamatwa katika mji wa Sirari zikisafirishwa kwa njia ya magendo.
----------------------------------------------------------
Katika ziara hiyo, RC Mtanda amekuta pikipiki 16 zikishikiliwa katika kituo cha Polisi Tarime na 11 katika kituo cha Polisi Sirari, baadhi zikiwa ni ambazo zilikamatwa katika matukio ya uhalifu yakiwemo ya kusafirisha dawa za kulevya na bidhaa nyingine kama vile saruji, mafuta ya kula na sabuni kwa njia ya magendo.
#Tuhakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment