NEWS

Thursday 2 November 2023

Timu ya riadha ya Barrick North Mara yaitangaza Tanzania mashindano ya Cape Town Marathon



Wachezaji wa timu ya Barrick North Mara Runners Club, wakifurahi baada ya kumaliza mbio ndefu za kilomita 42.2 katika mashindano ya Cape Town Marathon yaliyomalizika nchini Afrika Kusini, hivi karibuni.
------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
----------------------------


TIMU ya riadha ya Barrick North Mara Runners Club, inayoundwa na wafanyakazi wa mgodi wa Barrick North Mara, baada ya kushiriki mashindano mbalimbali ya ndani, sasa imezidi kuchanja mbuga na kushiriki mashindano ya kilomita 42.2 ya Sunlam Cape Town Marathon, yaliyomalizika nchini Afrika Kusini hivi karibuni, ambapo pia imepata fursa ya kuitangaza Tanzania katika mashindano hayo. 

Kepteni ya timu hiyo, Sarah Cyprian amesema wachezaji wote wa timu hiyo wako vizuri na wameweza kushiriki mbio hizo za umbali mrefu na kumaliza, na kwamba wamefurahi kushiriki mashindano hayo makubwa ya riadha ya kimataifa na kuitangaza Tanzania. 


Sarah akifurahi baada ya kumaliza mbio za kilomita 42.2 za Cape Town Marathon.

Sarah amesema kwamba kupitia mashindano hayo yaliyowakutanisha wakimbiaji kutoka nchi mbalimbali, wamejifunza mambo mengi na anaamini wameanza kupata uzoefu utakaowawezesha kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa watakayoshiriki siku za mbele. 

Ameeleza kuwa timu ya riadha ya Barrick North Mara Runners Club ilianzishwa mwaka 2016 na inajumuisha wakimbiaji 66, miongoni mwao wanaume wapo 53 na wanawake 13. 



Kepteni huyo ameyataja baadhi ya mashindano ambayo timu hiyo imeshiriki kuwa ni Kilimanjaro International Marathon -Moshi, Capital City Marathon –Dodoma (ilitoa mshindi wa tisa wa umbali wa kilomita 21), Serengeti Migration Marathon 21 km-Mugumu, Serengeti Safari Marathon 21km-Lamadi na Lake Victoria Marathon - Mwanza (ilitoa mshindi wa 4 kwa wanawake mbio za kilomita 21). 

Mashindano makubwa ambayo timu hiyo imeshiriki na kung’ara ameyataja kuwa ni Kilimanjaro International Marathon ambapo ilishiriki mbio za kilomita 21 na kilomita 42, ambapo kwa mbio hizo za masafa marefu ya kilomita 42, timu hiyo iliwakilishwa na yeye mwenyewe. [Sarah Cyprian]. 

Sarah akiendelea kufurahi.

Akielezea siri ya mafanikio ya timu hiyo, Sarah amesema: “Kampuni ya Barrick inayo sera mathubuti katika kusaidia wafanyakazi kwenye upande wa michezo. Kwanza kwa kuwa na miundombinu ya mazoezi kama gym, swimming pool, uwanja wa mpira wa miguu, uwanja wa mpira wa kikapu na uwanja wa mpira wa pete. Pia inatoa vifaa na nyenzo mbalimbali za kufanyia mazoezi, vilevile kugharimia huduma zote tunapoenda kwenye mashindano nje”. 

Ameongeza kuwa Kampuni ya Barrick pia kupitia kitengo cha Afya na Usalama huwa inaandaa mashindano ya ndani kwa kushindanisha idara mbalimbali kama njia mojawapo ya kuweka vizuri afya za mwili na akili za wafanyakazi wawapo kazini. 


Kuhusu ni jinsi gani wanaweza kutenga muda wa kazi na muda wa kufanya mazoezi, Sarah amesema: “Kila mtu ana saaa 24 za siku. Klabu ya North Mara Runners huwa tunatenga muda wa saa moja kwa siku kufanya mazoezi jioni mara baada ya kutoka kazini, na mara chache ratiba zinapokuwa zinabana jioni huwa tunafanya mazoezi saa kumi alfajiri kabla ya kwenda kazini.” 

Kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika mazoezi na kushiriki mashindano, amesema kulingana na majukumu ya kazi huwa kuna wakati ni vigumu wote kwenda kushiriki mashindano, lakini huwa wanajitahidi kutoa wawakilishi kwa ajili ya kushiriki mashindano, na kampuni huwa inawaunga mkono wakati wote. 



Akitoa maoni kuhusu maendeleo ya tasnia ya mchezo wa mbio za marathon nchini, Sarah amesema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mwitiko mkubwa katika mchezo wa mbio na kushauri kuwa ni vizuri kuanza maandalizi mapema kwa vijana wadogo ili kuweza kuwa na washiriki wengi katika mbio za kimataifa. 

Ameongeza kuwa kuna wakimbiaji wengi wenye vipaji nchini kwa sasa ambao wanashiriki mashindano ya marathon mbalimbali yanayoandaliwa nchini. 



Sarah ametoa wito kwa jamii kujitahidi kutenga muda hata nusu saa kwa siku kufanya mazoezi. “Mazoezi yanasaidia kuimarisha afya ya akili na mwili. Pia mazoezi yanasaidia kuweza kujikinga na magonjwa yasioambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na unene wa kupindukia,” amesema. 

Akizungumzia malengo ya baadaye ya klabu hiyo, Sarah amesema: “Kaulimbiu ya klub yetu ni ‘We run for fun and healthy’, hivyo basi bado tunajukumu la kuhimiza wafanyakazi wengi zaidi kufanya mazoezi kwa ajili ya afya zetu, kwani mazoezi pia yamekuwa yakituweka vizuri kiakili hata kuweza kutimiza majukumu yetu kazini kwa ufanisi zaidi. Lakini pia kuweza kushiriki zaidi katika marathoni za kimataifa.”

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages