Afisa Mwandamizi kutoka BoT, Omar Msuya akisisitiza jambo kwenye semia ya kutangaza fursa za biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa wafanyabiashara katika mji wa Sirari, jana Jumatano.
------------------------------------------------
Mara Online News
----------------------------
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza fursa za biashara ya kubadilisha fedha za kigeni (Bureau De Change (BDC)/ Forex Bureau) kwa wafanyabiashara mbalimbali wanaoendesha shughuli zao katika mji wa Sirari uliopo wilayani Tarime, Mara, mpakani na nchi ya Kenya.
Kupitia semina iliyofanyika kwenye ukumbi wa Idara ya Forodha Kituo cha Sirari jana Jumatano, maafisa waandamizi kutoka makao makuu ya BoT waliwafahamisha wafanyabiashara hao Kanuni Mpya za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni za Mwaka 2023.
Meneja Msaidizi Kitendo cha Huduma za Kifedha kwa Taasisi Maalum kutoka BoT, Omar Msuya alisema kanuni hizo zimeainisha makundi matatu ya leseni za biashara hiyo; ambayo ni daraja A, B na C.
“Daraja A kwa wamiliki wageni [wasio Watanzania] mtaji wake ni shilingi za Kitanzania bilioni moja na kwa wazawa ni shilingi milioni 500, daraja B ni kwa Watanzania tu kwa mtaji wa milioni 200 na daraja C pia ni kwa wazawa tu wenye mtaji wa hoteli,” alisema Msuya.
Mfanyabiashara maarufu katika mji wa Sirari, Joseph Nyabaturi akiuliza swali katika semina hiyo.
Kwa mujibu wa Msuya, wananchi wanaruhusia kuungana hadi watu sita kwa ajili ya kuanzisha biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa kutuma maombi BoT ambako hushughulikiwa ndani ya siku 30.
Alibainisha kuwa biashara ya kubadilisha fedha za kigeni husimamiwa na BoT kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Kigeni ya Mwaka 1992, ambayo imeipa benki hiyo mamlaka ya kutunga kanuni za kusimamia biashara hiyo.
Hivyo hata mameneja wa matawi/ maduka ya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni lazima waidhinishwe na BoT ili kuepusha kuvujisha siri za ofisi, alisema.
Msuya alitumia nafasi hiyo pia kuhamasisha wananchi kuwa na uthubutu wa kuanzisha biashara hiyo na kuepuka kutumia ‘vishoka’ na madalali kwani wanawaongezea gharama zisizo za lazima na kuchelewesha huduma husika kutoka BoT.
Semina hiyo ilihudhuriwa pia na Mnadhimu (Staff Officer) wa Mkoa wa Polisi Tarime Rorya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ame Anange ambaye aliwakumbusha wafanyabiashara kujenga utamaduni wa kushirikisha Jeshi la Polisi katika suala la ulinzi wa biashara zao.
Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni (BDC) inahusisha kuuza na kununua fedha za kigeni na kupeleka fedha nje kwa niaba ya wateja.
“Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment