Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Kailima Ramadhan akizungumza katika mkutano na wadau wa uchaguzi wilayani Rorya leo Novemba 20, 2023.
------------------------------------------------
Mara Online News
-------------------------------
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) leo imekutana na wadau wa uchaguzi wilayani Rorya, na kutangaza tarehe ya Uboreshaji wa Majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Kailima Ramadhan amesema shughuli hiyo itafanyika Novemba 24 hadi 30, mwaka huu katika vituo 16 vya kuandikisha wapigakura.
“Kati ya hivyo, vituo 10 vipo katika kata ya Ng’ambo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora mkoani Tabora, na sita vipo katika kata ya Ikoma, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara,” amefafanua Kailima katika sehemu ya hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo wa siku moja.
Wadau wa uchaguzi wakifuatilia mada katika mkutano huo.
Huku akiwapongeza wakazi wa maeneo hayo kwa kubahatika kuwa wenyeji wa shughuli hiyo, Kailima amesema lengo ni kuvifanyia majaribio vifaa na mfumo husika, ili kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza na kuzipatia ufumbuzi kabla ya kuanza rasmi kwa uboreshaji wa daftari hilo nchi nzima.
Amesema uboreshaji huo wa majaribio utahusisha kuandikisha raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18, au zaidi na watakaotimiza umri wa miaka hiyo kabla, au ifikapo taraehe ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
“Kundi lingine litakalohusika ni pamoja na wapigakura wanaoboresha taarifa zao ambao wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda lingine, waliopoteza au kadi zao kuharibika, wanaorekebisha taarifa zao na kuondoa wapigakura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura,” ameongeza.
Sehemu nyingine ya wadau wa uchaguzi katika mkutano huo.
Aidha, Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi amesema Tume imejipanga kutumia njia mbalimbali, vikiwemo vyombo vya habari kuhakikisha kuwa wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu uboreshaji wa majaribio wa daftari hilo.
“Katika eneo hili tunawategemea waandishi wa habari kushirikiana nasi kwa kutoa taarifa za uwepo wa shughuli hii, lakini pia kuwahamasisha wananchi kujitokeza katika vituo vya kuandikisha wapigakura,” amesema Kailima.
Katika mkutano huo, Tume pia imeweza kuwapitisha wadau hao katika mada inayohusu maandalizi ya Uboreshaji wa Majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapigakura, kabla ya wengi wao kutoa maoni na mapendekezo yanayolenga kufanikisha utekelezaji wa shughuli hiyo.
Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Kailima (wa pili kulia mbele) na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau walioshiriki mkutano huo wilayani Rorya.
No comments:
Post a Comment