NEWS

Thursday 30 November 2023

Wakutugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu: Tuliyoyaona mgodi wa Barrick North Mara ni tofauti na tunayoyasikiaWakurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa idara mbalimbali za mgodi wa Barrick North Mara, Jumanne iliyopita.
-----------------------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU,
Nyamongo
--------------------------


Timu ya Wakurugenzi watano kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM) imefurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara katika kutoa ajira kwa Watanzania, kuwezesha vijana kiuchumi na kufadhili miradi ya kijamii.

Wakurugenzi hao wenye dhamana ya masuala ya kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu, waliyasema hayo wakati wa ziara yao ya siku mbili iliyohitimishwa Jumanne iliyopita katika mgodi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.


Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu mara baada ya kuwasili na kupokewa katika mgodi wa Barrick North Mara.

“Niwapongeze sana, haya tuliyoona hapa ni tofauti na tunayoyasikia kuhusu huu mgodi. Michango yenu ni muhimu sana. Sisi ofisi ya Waziri Mkuu tunaweza kushirikiana kuwezesha vijana wajitambue na waone fursa zilizopo na kuzitumia kwa tija.

“Mmefanya mambo makubwa sana kwenye jamii, ikiwemo huu mpango wa kuwajengea vijana uwezo kujiajiri kupitia kilimo na ninyi kuwa sehemu ya soko la bidhaa wanazozalisha,” alisema Dkt Mwiga Mbesi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana.

Naye Mkurugenzi wa Ukuzaji Tija, Yohana Madadi ambaye alikuwa kiongozi wa msafara wa timu hiyo ya Wakurugenzi kutoka OWM, alieleza kuridhishwa na fursa za ajira, uwezeshaji vijana na miradi ya kijamii zilizotengenezwa na mgodi wa Barrick North Mara.

“Tumeona kazi kubwa ambayo mnaifanya kugusa jamii hadi kwenye ajira. Hii ni kazi kubwa sana,” alisema Yohana Madadi mara baada ya wote kupokea taarifa za idara za mahusiano ya jamii na rasilimali watu katika mgodi huo.


Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (kulia) katika kikao cha ndani na wakuu wa idara mbalimbali za mgodi wa Barrick North Mara.

Hadi sasa mgodi wa Barrick North Mara umeajiri watu 1,391 ambapo asilimia 96 kati yao ni Watanzania na asilimia 67 wanatoka katika vijiji vinavyouzunguka.

Hivyo idadi ya wageni ambao ni wataalamu (experts) walioajiriwa katika mgodi huo imepungua hadi asilimia nne. Aidha, mgodi huo unafanya kazi na wakandarasi 248 ambapo kati ya hao, asilimia 97.5 ni Watanzania.

Meneja Rasilimali Watu wa Barrick North Mara, Ivo Masanja alisema mgodi huo una mpango wa kuongeza idadi ya wafanyakazi wanawake, sambamba na kuendelea kuwashawishi Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi kurudi nyumbani na kuwapatia ajira.

Kwa upande wake Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi aliwaeleza Wakurugenzi hao kutoka OWM kuwa mahusiano yao na jamii inayowazunguka yameendelea kuimarika, huku akitaja mradi wa kilimo biashara waliuanzisha kuwainua vijana kiuchumi kama ya moja ya mafanikio yanayoshuhudiwa.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Dkt Mwiga Mbesi (katikati mwenye kofia) akisisitia jambo wakati yeye na wenzake walipotembelea mradi wa kilimo biashara uliowezeshwa na mgodi wa Barrick North Mara kwa ajili ya vijana katika kijiji cha Matongo.

“Tayari vijana wanaonufaika na mradi huu wa kilimo biashara wamepata mauzo ya shilingi milioi 164 na tunataka baadaye utumike kama shamba darasa,” alisema Uhadi.

Alisema asilimia 40 ya mbogamboga na viungo vinavyozalishwa katika mradi huo inauzwa katika mgodi wa Barrick North Mara kupitia Kampuni ya AKO, na asilimia 60 inauzwa kwenye masoko huria nje ya mgodi.

Kwa upande mwingine, Meneja huyo wa mahusiano alisema mgodi huo umeweka mfumo mzuri wa kupokea na kutatua malalamiko ya wananchi.

Hata hivyo, alitaja vitendo vya uvamizi (intrusions), uporaji wa mawe ya dhahabu, uharibifu wa miundombinu na uchimbaji wa madini usio halali kama matatizo makubwa yanaukabili mgodi huo kwa sasa.


Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wakipata maelezo kutoka kwa Afisa Maendeleo ya Jamii wa Barrick North Mara, Praygod Mushi kuhusu mradi wa maji uliowezeshwa na mgodi huo kwa ajili ya kusambaza huduma kwa vijiji vinavyouzunguka.

Katika tamko lao Wakurugenzi hao kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu waliahidi kushirikiana na mgodi wa Barrick North Mara kutunisha mfuko wa kuwezesha vijana kiuchumi, ili waweze kukidhi mahitaji yao na kuchangia maendeleo ya taifa.

Walisema hatua hiyo itasaidia kupunguza vitendo vya kuvamia mgodi huo vinavyofanywa na makundi ya watu wanaojulikana kwa jina la ‘intruders.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Dkt Mwiga, kwa sasa vijana wana fursa ya kupata mkopo wa hadi shilingi milioni 50 katika Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ulio chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Wakurugenzi wengine kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu walioshiriki ziara hiyo katika mgodi wa Barrick North Mara ni Amosi Nyandwi (Taarifa za Soko la Ajira), Joseph Nganga (Huduma za Ajira na Kissa Kilindu anayeshughulikia Ukuzaji Ajira.

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages