
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya CAG kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Charles Kichere, Ikulu jijini Dar es Salaam, Machi 30, 2026.
Dar es Salaam
--------------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Taarifa ya Utendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na Taarifa ya Mwaka ya Tathmini ya Utendaji Kazi wa Ununuzi wa Umma (PPRA)
Kiongozi huyo wa nchi alikabidhiwa ripoti na taarifa hizo katika hafla iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam, Machi 30, 2026.

Rais Samia akipokea Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa TAKUKURU kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Crispin Chalamila.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, uadilifu na usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma - misingi ambayo ni nguzo muhimu katika kuimarisha utendaji wa serikali na kuharakisha maendeleo ya taifa.
Alipongeza kazi inayofanywa na taasisi hizo katika kuimarisha uwazi na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, akisema juhudi hizo zinaendelea kulinda rasilimali za taifa na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Rais Samia akipokea Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa PPRA kutoka kwa Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Dennis Simba.
"Nimesikiliza taarifa zilizowasilishwa na taasisi zetu, na ninaendelea kusisitiza kuwa uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma si jambo la hiari, bali ni wajibu wa msingi kwa kila kiongozi na mtumishi wa umma," alisema Rais Samia.
Akizungumzia ripoti ya CAG, alisema tathmini hiyo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma, akibainisha kuwa serikali imepokea na itazifanyia kazi hoja za ukaguzi kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Rais Samia akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kupokea Ripoti ya CAG, Taarifa ya TAKUKURU na Taarifa ya PPRA.
Kwa upande wa ripoti za TAKUKURU na PPRA, Rais Samia alisema zimeonesha hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, kuongeza uwazi katika manunuzi ya umma na kuimarisha nidhamu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Vilevile, Rais alipongeza matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), akisema umeongeza uwazi na ushindani katika manunuzi ya serikali.
Aliagiza kuimarishwa kwa matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi na ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma.
"Tuendelee kuimarisha mifumo ya kidigitali na ya usimamizi ili kuongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma," alisema Rais Samia.

Wakati huo huo, Rais Samia amekemea vitendo vya uzembe, ubadhirifu na matumizi yasiyo sahihi ya rasilimali za umma, na kutoa onyo dhidi ya vitendo vya makusudi vinavyokwamisha juhudi za maendeleo ya taifa.
"Kila kiongozi na mtumishi wa umma ana wajibu wa kuhakikisha rasilimali za taifa zinasimamiwa kwa uadilifu, kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya nchi yetu," alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amezitaka taasisi za umma kuchukua hatua kwa wakati kushughulikia hoja zilizobainishwa, akisisitiza kuwa utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti hizo utaimarisha uwajibikaji, kulinda rasilimali za taifa na kuongeza ufanisi wa serikali katika kuwahudumia wananchi.
Ripoti ya CAG imeonesha kuwa deni la Taifa linaendelea kuwa himilivu, likizingatia uwezo wa serikali kulihudumia pamoja na mwenendo wa ukuaji wa uchumi na mapato ya ndani.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere akisoma Muhtasri wa Ripoti yake kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, mbele ya Rais Samia..
Ripoti ya CAG pia imebainisha ongezeko la hati safi kwa taasisi za umma, hali inayoashiria kuimarika kwa uwajibikaji, uwazi na usimamizi wa rasilimali za umma.
Kwa upande wa ununuzi wa umma, kwa mara ya kwanza Taarifa ya Mwaka ya Tathmini ya Utendaji Kazi wa Ununuzi wa Umma imewasilishwa kwa Rais, hatua inayolenga kuimarisha uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma.
No comments:
Post a Comment