NEWS

Sunday 19 November 2023

Wamarekani waadhimisha na kusherehekea “Siku ya Tanzania” jijini Milwaukee



Mkurugenzi Mkuu wa Mosorec International Foundation, Inc. Dr Christine Mosore (wa nne kulia) na washiriki/ wageni wengine wakiwa katika maadhimisho ya "Siku ya Tanzania" jijini Malwaukee, Marekani hivi karibuni.
--------------------------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU,
Milwaukee – Marekani
---------------------------------


KAMPUNI ya Kimarekani ijulikanayo kama Mosorec International Foundation iliyoko jijini Milwaukee, Wisconsin imeandaa na kuadhimisha kwa mara ya kwanza “Siku ya Tanzania”, ambapo wageni waalikwa waliweza kufurahia ukarimu, utamaduni na burudani za Kitanzaia.

“Hafla hiyo maalum ambayo ilijumuisha kila mtu aliyependa kushiriki, ilifanyika Novemba 9, 2023 katika jengo la Jiji la Milwaukee (City Hall) na watu walijawa na bashasha, hususan pale Meya wa Jiji hilo, Cavalier Johnson alipoitangaza rasmi Novemba 9 kila mwaka kuwa “Siku ya Tanzania,” anaeleza Mwanzilishi, Rais na Mkurugenzi Mkuu wa Mosorec International Foundation, Inc. Dkt Christine Mosore.

Vyakula, muziki, elimu, burudani na maonesho ya mavazi ya Kitanzania vilikuwa vivutio vikubwa katika sherehe hizo.

Wanafunzi wengi kutoka shule mbalimbali za jijini Milwaukee walihudhuria sherehe hiyo na walipata pia fursa ya kutembelea maeneo kadhaa ya jengo la jiji.

“Kilichonifurahisha zaidi ni kuona wageni wengi, hasa wanafunzi kutoka jiji la Milwaukee walivyoshiriki na kufurahia,” anasema Dkt Mosore.

“Siku ya Tanzania” ilisherehekewa sambamba na maadhimisho ya Miaka Saba ya Jiji la Milwaukee na Wilaya ya Tarime nchini Tanzania, ambao wana uhusiano wa kindugu ulioanzishwa November 7, 2016.

Salaamu nyingi za pongezi zilitoka kwa Meya wa Jiji la Milwaukee, Cavalier Johnson na Gavana wa Wisconsin, Tony Evers.

Wengine waliotuma pongezi zao ni Mjumbe wa Baraza la Congress, Gwen Moore, Seneta wa Jimbo la Wisconsin, Lena Taylor, Mwenyekiti wa Kamati ya Miji ya undugu ya Milwaukee, Alderman Russell Stamper II, Baraza la Jiji la Milwaukee na maafisa wengi wa kuchaguliwa pamoja na viongozi wa kijamii.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages