NEWS

Sunday 24 December 2023

Barrick North Mara wavipatia vituo vya kulea watoto zawadi za Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, wagonjwa na wazee wa mila nao watabasamu



Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko (kushoto mbele), akikabidhi zawadi ya sikukuu katika kituo cha Kulea Watoto cha Hope of City wilayani Tarime jana.
----------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Tarime
---------------------------------------------


MGODI wa Dhahabu wa North Mara umevipatia vituo vya kulea watoto, hospitali na wazee wa mila wilayani Tarime zawadi mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya wa 2024.

Vituo vya kulea watoto vilivyopewa zawadi hizo jana ni Angel House, City of Hope na ATFGM Masanga ambavyo kila kimoja kimepata mbuzi wawili, mchele kilo 100, sukari kilo 100, maharage kilo 100, unga wa mahindi kilo 100, mafuta ya kula, chumvi, soda, juice na biskuti.

Misaada mingine ya soda, juice na biskuti ilielekezwa kwenye Kituo cha Afya Nyangoto (Sungusungu) na Hospitali ya Wilaya Nyamwaga kwa ajili ya wagonjwa.


Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko (katikati), akikabidhi zawadi za sikukuu katika Kituo cha Kulea Watoto cha Angel House wilayani Tarime jana.
-----------------------------------------------

Kwa upande wao, wazee wa mila kutoka koo za Wairege, Wanyabasi na Wanyamongo, pamoja na Umoja wa Koo 12 za kabila la Wakurya waliitikia wito wa kupokea zawadi hizo katika ofisi za Mahusiano za mgodi huo juzi.

Waliongozwa na Mwenyekiti koo 12 za kabila la Wakurya, Sylvanus Mtatiro kupokea zawadi hizo; ambazo koo hizo tatu kila moja ilipata ng’ombe mmoja, mchele kilo, sukari, unga wa mahindi, mafuta ya kula, chumvi na shilingi 500,000, na vivyo hiyo kwa Umoja huo wa koo 12.

Wazee hao, viongozi na watoto wa vituo vilivyopata misaada hiyo waliushukuru mgodi wa North Mara na kuumbea mafanikio makubwa katika shughuli za uchimbaji madini.

“Tunawashukuru sana, Mungu abariki kazi za mikono yenu na kuwawekea ulinzi,” Msimamizi wa Kituo cha Kulea Watoto cha Angel House, Nuru Anthony aliuambia uongozi wa mgodi huo.

Nao Chacha Yusuf Marwa na Emmy Wilfred walishukuru kwa niaba ya watoto wenzao wanaohudumiwa kituoni hapo, waliushukuru mgodi huo kwa kuwajali na kujitolea kuwapatia mahitaji hayo ya sikukuu.

“Mungu awabariki na kuwazidishia mlipotoa,” alisema Chacha, na Emmy akaongeza: “Tutaendelea kuwaombea baraka za Mungu.”


Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko (kulia mbele), akikabidhi zawadi za sikukuu katika Kituo cha ATFGM Masanga wilayani Tarime jana.
-----------------------------------------------

Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo, Meneja Mkuu (GM) wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko alisema wanapenda kuona uhusiano wao na jamii unaendelea kuimarika.

“Tumeona ni muhimu kusherehekea na kufurahia sikukuu hizi pamoja na jamii,” alisema GM Lyambiko na kuwapongeza walimu kwa kuwalea vizuri watoto vituo hivyo.

Alitumia nafasi hiyo pia kuwahimiza watoto wanaohudumiwa na vituo hivyo kudumisha nidhamu kwa walimu na walezi wao, na kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao.

Kwa upande mwingine, GM Lyambiko aliwashukuru na kuwaomba wazee wa mila kuendelea kukemea vitendo vya uvamizi mgodini vinavyofanywa na makundi ya watu hasa vijana.


Mwenyekiti wa koo 12 za kabila la Wakurya, Sylvanus Mtatiro (wa nne kulia mbele), akitoa neno la shukrani mara baada ya yeye na wenzake kupokea zawadi za sikukuu kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara wilayani Tarime jana. Wa pili kulia ni Meneja Mkuu wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko, na kulia ni Meneja Mahusiano wa mgodi huo, Francis Uhadi.
--------------------------------------------

“Nipende kuwashukuru sana wazee wetu kwa kazi kubwa ya kuelimisha jamii. Tuendelee na juhudi hizo ili kuhakikisha tunakomesha hii tabia [ya kuvamia mgodi],” GM Lyambiko aliwambia wazee hao wa mila na kuwatakia heri ya Krismasi na Mwaka Mpya wa 2024.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime, unaendeshwa na Kampuni ya Barrick Gold kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Mwaka jana, mgodi huo pia ulivipatia vituo vya kulea watoto vya Angel House na City of Hope msaada wa mahitaji mbalimbali kwa ajili ya kusherekea Sikukuu za Kristmasi na Mwaka Mpya.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages