Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele (mwenye fulana) na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Mwl Saul Mwaisenye (kushoto) wakiongoza kazi ya kung'oa zao haramu la bangi kijijini Kewamamba mapema leo Jumamosi.
----------------------------------------------------
Mara Online News, Tarime
------------------------------------
KAMATI ya Ulinzi na Usalama (KUU) Wilaya ya Tarime mkoani Mara, imefyeka mashamba kadhaa ya zao haramu la bangi - yenye ukubwa wa takriban ekari 20 katika kijiji cha Kewamamba wilayani hapa.
Shughuli hiyo imefanyika mapema leo Jumamosi - ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kanali Michael Mntenjele, akisaidiana na Katibu Tawala wa Wilaya, Mwl Saul Mwaisenye.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la tukio, Kanali Mntenjele ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, ametoa wito kwa wananchi wanaolima bangi wilayani hapa kuachana na kilimo hicho, la sivyo watarajie kushukiwa na rungu la dola.
Amesema operesheni ya kusaka wakulima wa bangi na kuteketeza mashamba ya zao hilo ni endelevu, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kilimo hicho kinatokomezwa wilayani Tarime.
Kanali Mntenjele akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).
-------------------------------------------
“Niendelee kutoa msisitizo kwamba wananchi waache kulima bangi. Tutaendelea kupambana na walima bangi ili kuhakikisha wanakoma kulima zao hili. Hatutakata tamaa wala kuishiwa nguvu. Tarime bila bangi inawezekana,” amesema Kanali Mntenjele.
No comments:
Post a Comment