NEWS

Saturday, 23 December 2023

Bodi ya WAMACU yabariki biashara ya mahindi, ununuzi wa magari



Bodi wa WAMACU ikiendelea na kikao chake mjini Tarime jana.
----------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News
--------------------------


BODI ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara Cooperative Union (WAMACU Ltd) imeidhinisha utekelezaji wa mpango wa biashara ya mahindi kwa mwaka 2024/2025.

Mpango huo ulipata baraka jana Ijumaa katika kikao cha Bodi ya WAMACU kilichofanyika mjini Tarime, chini ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo, David Hechei.
Aidha, kikao hicho kilipitisha mpango wa ununuzi wa magari mawili kwa ajili ya kusafirisha kahawa kutoka kituo kimoja hadi kingine, na mengine wawili ya ofisi kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za ushirika huo ili kuongeza ufanisi.

Hechei aliwataka watumishi wa WAMACU Ltd kufanya kazi kwa bidii huku wakitumia teknolojia katika uendeshaji wa shughuli za ushirika, ikiweo maandalizi ya taarifa za utendaji wake.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye alisema wamejipanga kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo na masoko mazuri ya mazao yao, huku akigusia mpango wa kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani.

“WAMACU tumeweka nguvu kubwa kwenye pembejeo za kilimo na masoko kwa mkulima, hiyo itaongeza uzalishaji wa mazao,'' alisema Gisiboye.

Upanuzi wa kilimo cha mahindi katika mkoa huo ulipata msukumo mkubwa katika kikao hicho.

Mjumbe wa Bodi hiyo na Mwenyekiti wa Jukwaa la Vyama vya Ushirika mkoani Mara, Momanyi Range alitoa wito kwa wakulima wa mahindi kulima zao hilo kwa wingi ili kujikwamua kiuchumi.

“Wito wangu kwa wakulima sasa waongeze uzalishaji, huduma zitakuwa karibu, hakuna atakayehangaika kwenda kutafuta soko Nchi jirani,” alisema Range.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages