NEWS

Friday 22 December 2023

Namba Tatu, Waitara wanyukanaSamwel Kiboye "Namba Tatu"
------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News
----------------------------


SASA ni ‘piga nikupige’. Ndivyo tunavyoweza kuelezea mnyukano wa maneno uliotokea kati ya Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara aliyepita, Samwel Kiboye - maarufu kwa jina la Namba Tatu.

Jana Alhamisi, ikiwa ni siku moja baada ya Waitara kutumia jukwa la kisiasa wilayani Rorya kumshambulia kwa maneno, Namba Tatu aliitisha mkutano na waandishi wa habari mjini Tarime kujibu mapigo kwa ‘kumponda’ vikali mbunge huyo.

“Namuonya Waitara na wenzake wasiniseme kwenye majukwaa, wakae kimya, waache kuchonganisha na kupotosha wananchi,” alisema Namba Tatu.

Huku akitishia ‘kumvua nguo’ Waitara, Namba Tatu alidai kuwa mbunge huyo ameshanusa harufu ya anguko. “Waitara ameshajua kwamba anakwenda kushindwa kwenye jimbo lake… nitasema mabaya yake, asinichezee,” alisema.


Mwita Waitara
-----------------------
Namba Tatu alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa viongozi wa CCM Mkoa wa Mara kupuuza ushauri wa Waitara kwani “atawaingiza shimoni”.

Juzi Jumatano, Waitara akizungumza katika mkutano wa hadhara wilayani Rorya, alimpiga vijembe Namba Tatu akimtuhumu kwamba alijaribu ‘kumshika miguu’ katika mchakato wa kuelekea kugombea ubunge mwaka 2020. “Alinipinga akiwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa,” alisema.

Waitara alikwenda mbali zaidi kwa kuahidi kupambana hadi kuwashinda mahasimu wake wa kisiasa. “Dawa ya mhuni ni kuwa mhuni zaidi, dawa ya moto ni moto,” alisema mbunge huyo kutoka chama tawala - CCM.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages