NEWS

Monday 18 December 2023

Kampuni ya Grumeti Reserves ilivyoinua ushirika wa GHOMACOS wilayani Serengeti



Wanachama wa GHOMACOS wakiuza mbogamboga na matunda katika soko la wilayani Serengeti. Bidhaa hizo ni ambazo wanazalisha kwenye ushirika wao huo.
-------------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Serengeti
-------------------------------------------------


MOJAWAPO ya changamoto zilizokabili maeneo yanayounda Grumeti Reserves Ltd wakati wa kuanzishwa kwake wilayani Serengeti - zaidi ya miaka 20 iliyopita, ilikuwa ni jinsi gani ingeweza kuendesha shughuli zake ilhali palikuwa na kiwango kikubwa cha ujangili na umasikini wa kipato katika jamii jirani.

Ujangili ulikuwa umesababisha madhara makubwa ya kimazingira - na hii ilikuwa ni changamoto kubwa kwa afya na ustawi wa Mapori ya Ikorongo na Grumeti ambamo kwa makubaliano na Serikali, Kampuni ya Grumeti Reserves ilipewa dhamana kuendesha shughuli zake.

Katika hali hiyo ni dhahiri, wanavijiji walihitaji chanzo halali cha kipato, hivyo utatuzi ulikuwa hauna budi kupatikana kwa haraka, kwani mafanikio katika uhifadhi hutegemea sana mchango na uungwaji mkono na jamii.

Pamoja na mambo mengi ikiwemo kuwapatia ajira wakazi wa maeneo jirani, ili kupunguza utegemezi huo wenye madhara makubwa, Kampuni ya Grumeti Reserves kwa kushirikiana na Serikali, wadau wengine wa maendeleo na uhifadhi hasa Grumeti Fund ilianzisha Chama cha Ushirika wa Wakulima na Wauzaji wa Mbogamboga na Matunda (GHOMACOS) mwaka 2010, kwa mujibu wa afisa mmoja mwandamizi wa Grumeti Fund.

Hatua hiyo muhimu imeleta manufaa na soko la uhakika kwa ajili ya mazao ya wakulima hao, hii ikiwa ni kwenye kampuni ya Grumeti na wadau wake, ambapo wafanyakazi zaidi ya 900, wageni mbalimbali, na watalii wanaokuja kutembelea eneo hilo wamekuwa watumiaji wakubwa wa bidhaa za mboga na matunda zinazozalishwa na kusambazwa na umoja huo.

Mpango huu wa kusaidia wakazi wa maeneo haya ulianzishwa kwa kutoa mafunzo ya kilimo na biashara na ufadhili wa pembejeo pamoja na namna bora ya kuendesha vikundi kama hivi.

Katika miaka ya hivi karibuni maboresho yamejumuisha mafunzo zaidi ya ujasiriamali, ukuzaji shughuli za kuongeza kipato na mikopo nafuu ili kuharakisha maendeleo na biashara endelevu.

Kwa sasa GHOMACOS imepanuka na kuwa asasi kubwa ya kilimo, inayojumuisha biashara ndogo ndogo na ukubwa wa kati - zinazojali utunzaji wa mazingira, tija, matumizi bora ya rasilimali, na wakati huo huo wanachama wake wakiendelea kunufaika na uendeshaji huru wa shughuli zao za kifedha.

“Najivunia GHOMACOS, imebadilisha maisha yangu, nimejenga nyumba na shamba langu linakua,” anasema Mwita Chacha ambaye awali alikuwa akijishughulisha na ujangili.

Anna Mohamed, mama wa familia ya watoto kadhaa, ni miongoni mwa wanachama wa GHOMACOS wanaofurahia matunda ya ushirika huo.

Amina ni mkazi wa kijiji cha Natta - miongoni mwa wananchi wa wilaya hiyo ambao wanaishi jirani na ikolojia ya Serengeti mkoani Mara.

“Niliingia GHOMACOS mwaka 2010 na mimi ni mkulima wa mboga na matunda. Nimeweza kusomesha watoto wangu na sasa wengine watatu wamepata kazi na wengine wanaendelea na masomo yao,” anasema Amina.

Anaongeza kuwa hatasahau msaada wa Kampuni ya Grumeti Reserves kwa kubadilisha maisha yao kupitia ushirika wa GHOMACOS. “Kwa kweli tunashukuru sana Kampuni ya Grumeti Reserves, siku hizi tuna uhakika wa kula na kupata mahitaji mengine muhimu,” anasema.

Taarifa zinasema ushirika huo hivi sasa umeweza kuajiri watumishi na kuwalipa msahara bila kutegemea Kampuni ya Grumeti kama ilivyokuwa mwanzo.

Viongozi wa kijamii akiwemo Diwani wa Kata ya Natta-Mbisso, Juma Porini, wanasema ushirika huo wa GHOMACOS umesaidia kugusa maisha wa wananchi wengi kwenye ukanda wa Grumeti.

“Wengi wa wanachama wa GHOMACOS wamejenga na wanasomesha watoto kutokana na mapato yanayotokana na bidhaa wanazozalisha,” anasema.

Porini anasema sio tu kwamba wanatoka katika vijiji vya kata ya Natta-Mbisso bali katika kata jirani kama vile Kyambahi, Nagusi na Issenye.

Kwa mujibu wa diwani huyo, Kampuni ya Grumeti Reserves kwa ushirikiano na Grumeti Fund imekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea uwezo wanufaika wa GHOMACOS juu ya kusimamia ushirika wao na hivyo kujiendesha kwa faida.

“GHOMACOS imeendelea kukua na hata wamenunua mashine ya kufungasha unga na hivi karibuni nimefanya nao ziara ya kutafuta masoko katika moja ya hoteli zilizopo katika Hifadhi ya Taifa Serengeti,” anaongeza Diwani Porini.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages