NEWS

Monday 4 December 2023

Mawaziri wafika eneo la maafa ya maporomoko ya tope Hanang kusimamia hatua za dharura
Na Mwandishi
Wetu, Hanang
-------------------------


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakiwa wameambatana na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wamefika katika kijiji cha Gendabi wilayani Hanang, Manyara yalikotokea mafuriko na maporomoko ya tope na kusababisha vifo vya makumi ya watu, majeruhi na uharibifu mkubwa wa miundombinu mbalimbali, yakiwamo mashamba na makazi ya wananchi.

Baada ya kuwasili leo Desemba 4, 2023, viongozi hao wameongozwa na Mkuu wa Mkoa Manyara, Queen Sendiga kufika katika Kijiji hicho kilichoathirika zaidi na maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanang usiku wa kuamkia jana Desemba 3, 2023.

Mara tu baada ya kuwasili, Waziri Mhagama amewasilisha kwa wakazi wa Kijiji hicho salamu za pole kutoka kwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye aliwaagiza kufika eneo la tukio na kuona nini kifanyike kwa dharura kuhusu uokoaji na makazi kwa waathirika wa maafa hayo.


“Mambo haya yakitokea kuna mambo ya haraka yanatakiwa yafanyike kwa dharura, hivyo tumekuja na kushauriana namna ya kujipanga kwa pamoja ili kufanikisha jambo hilo kwa uharaka,” ameongeza Waziri Mhagama.

Ameongeza kuwa maelekezo ya Rais Samia kwanza ni kuona namna gani nzuri Zaidi ya kuendelea kuokoa watu, kazi ambayo vikosi vya uokozi vinaendelea nayo, lakini pia kuangalia namna ya kuwasitiri watu waliopoteza maisha.

Aidha, Waziri huyo amesema Serikali imeshapeleka wataalamu wa miamba watakaotoa taarifa ya kilichotokea na nini kifanyike katika mlima Hanang.

Kwa upande wake Waziri Bashungwa amesema kazi ya kufungua miundombinu ya barabara inaendelea ili kurahisisha kazi za uokoaji na kufikisha huduma muhimu za kijamii katika meneo yaliyoathirika.

Amesema Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imefungua Barabara ya Singida-Babati ambayo awali ilikuwa haipitiki kutokana na kujaa tope na magogo ya miti kutoka mlimani.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages